Wakati ikiwa imetimia miaka minne ya uongozi wa Rais wa Tanzania Dk Samia Suluhu Hassan tayari maendeleo katika sekta mbalimbali nchini yameonekana kwa kiasi kikubwa kama ilivyo azma yake ya maendeleo na ustawi wa nchi.
Moja ya sekta hizo ni ujenzi ambapo kupitia Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), kumeshuhudiwa maendeleo makubwa ambapo Serikali imefanikiwa kutekeleza miradi mingi ya ujenzi wa majengo kwa ajili ya sekta za afya, ofisi, makazi ya viongozi na watumishi wa umma kwa ubora unaotakiwa.
Hatua hiyo ya kutekeleza miradi hiyo mikubwa, inatajwa kuongeza wigo wa kutoa huduma na kurahisisha utendaji kazi katika sekta hizo. Utekelezaji wa miradi hiyo ni kama ifuatavyo:
Miradi ya kimkakati
Serikali imeendelea kutekeleza miradi mikubwa ya kimkakati ambapo kupitia TBA imefanya usimamizi wa miradi ya ujenzi wa vihenge vya kisasa na maghala ya kuhifadhia nafaka katika mikoa minane nchini. Mikoa hiyo inajumuisha Dodoma, Shinyanga, Katavi, Rukwa, Songwe, Njombe, Ruvuma na Manyara ambapo tayari mradi katika mikoa ya Manyara, Katavi na Rukwa imeshafunguliwa na Rais kwa nyakati tofauti.
Utekelezaji wa mradi huo ni moja ya jitihada za Serikali za kukuza uchumi kwa wakulima na kuchochea maendeleo ya viwanda pamoja na kuongeza uwezo wa uhifadhi wa chakula nchini.

Muonekano wa nyumba za kupangisha zilizopo katika eneo la Sekei jijini Arusha.
Pia, Serikali imefanikiwa kutekeleza mradi wa ujenzi wa jengo la Ofisi ya Rais Ikulu Chamwino ambapo TBA imefanya ubunifu wa jengo hilo ambalo ni jengo pacha na jengo la Ofisi ya Rais Ikulu Dar es Salaam na kusimamia ujenzi wake ambao umekamilika kwa asilimia 100. Ofisi ya Ikulu Chamwino ilifunguliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dk Samia Suluhu Hassan Mei 20, 2023 Jijini Dodoma.
Vilevile, Serikali imefanikiwa kutekeleza mradi wa ujenzi wa mji wa Serikali Mtumba awamu ya pili ambapo TBA imefanya ubunifu wa majengo yote na sasa inasimamia ujenzi wa majengo 17 ya wizara na taasisi 4 na kujenga jengo moja la Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kama Mkandarasi ambalo tayari limeshakamilika na kuanza kutumika.
Pia, Serikali kupitia TBA inasimamia mradi wa ujenzi wa Kituo cha Pamoja cha Forodha (OSBP) kilichopo Kasumulu mpakani mwa Tanzania na Malawi. Mradi huo uliwekwa jiwe la msingi na Dk Samia mnamo Agosti 07, 2022.
Aidha, pamoja na miradi hiyo TBA inaendelea na usimamizi wa miradi ya ukarabati wa viwanja vya michezo vya Benjamini Mkapa na Uhuru jijini Dar es Salaam.
Miradi ya fedha za ruzuku
Katika kipindi cha hii miaka minne Serikali kupitia TBA imefanikiwa kutekeleza miradi mbalimbali kwa kutumia fedha za ruzuku. Miradi hiyo inajumuisha mradi wa ujenzi wa nyumba za makazi za Magomeni Kota awamu ya kwanza ambapo kaya 644 tayari zinaishi.
Ujenzi wa nyumba hizo ulienda sambamba na ujenzi wa maduka ya kisasa na soko la wafanyabiashara wadogo (machinga) kwa ajili ya kutoa huduma kwa wakazi wanaoishi katika nyumba hizo.
Upo pia, mradi wa ujenzi wa nyumba 3500 za watumishi wa umma katika eneo la Nzuguni ‘B’ Jijini Dodoma ambao uliwekwa jiwe la msingi na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dk Philip Mpango Novemba 30, 2022.
Serikali imefanikiwa kutekeleza mradi huo ikiwa ni hatua ya kupunguza uhaba wa nyumba kwa watumishi mbalimbali wa Umma jijini humo kwa kuanza awamu ya kwanza ya ujenzi wa nyumba 150 ambazo zimeshakamilika na kuanza kutumika.
Vilevile, awamu ya pili ya ujenzi wa nyumba nyingine 150 umefikia asilimia 27. ujenzi wa nyumba hizo 3500 utajumuisha ujenzi wa maghorofa 100 aina ya Villa yenye ukubwa wa mita za mraba 335 kila moja, nyumba kubwa 200 aina ya Bungalow zenye ukubwa wa mita za mraba 190 kila moja, nyumba 300 za saizi ya kati zenye ukubwa wa mita za mraba 100 kila moja, maghorofa yenye jumla ya nyumba 800 za ukubwa tofauti tofauti, maghorofa yenye jumla ya nyumba 1000 za ukubwa wa mita za mraba 100 kwa kila nyumba na huku nyumba 1100 zikiwa za saizi ya kati zenye ukubwa wa mita za mraba 120 kila moja.
Pamoja na uwepo wa nyumba hizo, pia eneo hilo kutakuwa na huduma mbalimbali za kijamii ambapo kutajengwa shule tano za awali, nyumba za ibada (misikiti na makanisa), kituo cha biashara, kituo cha afya, kituo cha polisi, eneo la michezo, eneo la mapumziko, barabara na mandhari ya nje.
Aidha, mradi mwingine uliotekelezwa kupitia fedha za ruzuku ni ule wa ujenzi wa nyumba 20 za viongozi katika eneo la Kisasa jijini Dodoma. Mradi huo umekamilika na umepunguza uhaba wa nyumba za makazi ya viongozi uliojitokeza mara baada ya Serikali kuhamishia makao yake makuu jijini Dodoma.
Upo pia, mradi wa ujenzi wa majengo mawili ya ghorofa manane yenye uwezo wa kuchukua familia 16 kwa kila jengo moja kwa ajili ya makazi ya watumishi wa umma katika eneo la Magomeni kota. Miradi hiyo imetekelezwa katika awamu ya pili ambayo tayari imeshakamilika na kuanza kutumika.
Jengo la awamu ya kwanza lilifunguliwa rasmi Machi 29, 2023 na Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi (wakati huo) Mhe. Prof. Makame Mbarawa. Pia jengo la awamu ya pili lilifunguliwa rasmi Julai 23, 2024 na Waziri wa Ujenzi (wakati huo) Mhe. Innocent Bashungwa.
Pia TBA inaendelea na utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa majengo mengine mawili ya ghorofa nane yenye uwezo wa kuchukua familia 16 kila moja kwa ajili ya watumishi wa umma katika eneo hilo la Magomeni Kota ambayo yamefikia asilimia 35 na 20.
Katika eneo la Temeke Kota mradi wa ujenzi wa nyumba za watumishi wa umma unaendelea na sasa umefikia asilimia 40 ya utekelezaji. Vilevile Serikali kupitia TBA imefanikiwa kukamilisha ujenzi wa nyumba nne za majaji katika Mikoa ya Tabora, Kilimanjaro, Mtwara, na Shinyanga.
Na pia, TBA imefanikiwa kukamilisha miradi ya ukarabati wa nyumba za Serikali zinazosimamiwa na TBA kwa lengo la kuboresha makazi na kuchochea uwajibikaji kwa watumishi na viongozi kwa umma.
Aidha, katika kipindi cha miaka minne ya Dk Samia, Serikali kupitia TBA imefanikiwa kuanza utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa jengo la ghorofa saba lenye uwezo wa kuchukua familia 14 kwa ajili ya makazi ya watumishi wa Umma katika eneo la Ghana Kota jijini Mwanza ambalo limefikia asilimia 25 ya utekelezaji.
Miradi iliyotekelezwa kwa fedha za mapato ya ndani
Katika hii miaka minne, Serikali kupitia TBA imetekeleza miradi kwa fedha za mapato za ndani. Miradi hiyo inajumuisha ujenzi wa jengo la makazi la Biashara katika eneo la Simeon jijini Arusha lenye uwezo wa kuhudumia familia 22 lililokamilika na kuzinduliwa na Makamu wa Rais wa Tanzania Mhe. Dk Philip Mpango Agosti 04, 2023.
Miradi mingine inajumuisha ujenzi wa jengo la makazi la ghorofa sita lenye uwezo wa kuchukua familia 12 katika eneo la Ex- Canadian Masaki ambalo limeshakamilika na sasa linatumika. Jengo hilo lilifunguliwa rasmi Machi 29, 2023 na Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi (wakati huo) Mhe. Prof. Makame Mbarawa. Pia, TBA inaendelea na ujenzi wa majengo mawili ya ghorofa sita yenye uwezo wa kuchukua familia 12 kila moja katika eneo hilo ambapo utekelezaji wake umefika asilimia 80 na 65.
Katika eneo la Ghana Kota jijini Mwanza, TBA inaendelea kutekeleza mradi wa ujenzi wa jengo la makazi la ghorofa sita lenye uwezo wa kuchukua familia 12 ambalo limefikia asilimia 50 ya utekelezaji.
Vilevile kwa kutumia fedha za mapato ya ndani, Serikali kupitia TBA imefanikiwa kutekeleza mradi wa ujenzi wa nyumba tatu kila mkoa ambazo zimejengwa katika mikoa ya Simiyu, Morogoro, Rukwa na Katavi.
Aidha, TBA imefanikiwa kutekeleza mradi wa Ujenzi wa nyumba 12 za watumishi wa Umma katika mkoa wa Mtwara, nyumba tatu katika Mkoa wa Tanga, nyumba nane katika Mkoa wa Pwani pamoja na kukarabati nyumba za watumishi wa umma katika maeneo mbalimbali nchini. Vile vile, TBA inaendelea kutekeleza mradi wa ujenzi wa nyumba 16 za watumishi wa Umma katika Mkoa wa Mtwara ambapo utekelezaji wake umefikia asilimia 25.
Majengo ya ofisi na hospitali
Katika kipindi hiki cha miaka minne ya uongozi wa Dk Samia madarakani, TBA imefanikiwa kutekeleza miradi mbalimbali ya washitiri. Miradi hiyo inajumuisha miradi ambayo inatekelezwa na TBA kama Mkandarasi au mkandarasi na mshauri elekezi au mshauri elekezi pekee au msimamizi wa mradi (project manager).
Miradi hiyo inajumuisha Mradi wa ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda, Chato. Mradi huo ulitembelewa na Rais Dk Samia, Oktoba 15, 2022. Miongoni mwa majengo yaliyojengwa kwenye hospitali hiyo katika awamu ya kwanza na ya pili ni pamoja na jengo la wagonjwa wa nje (OPD), jengo la Mionzi, jengo la famasi pamoja na jengo la dharura.
Pia TBA inaendelea na ujenzi wa jengo la wodi ya kulaza wagonjwa ambalo ujenzi wake umefikia asilimia 89 huku awamu ya tatu ya ujenzi wa majengo ya mochwari, sehemu ya kufulia na kutakasia vifaa tiba, jengo la kuzalishia hewa tiba ikiwa imefikia asilimia 68.
Vilevile, Serikali kupitia TBA imekamilisha ujenzi wa jengo la Huduma ya afya ya Mama na mtoto katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mwanza Sekou-Toure ambapo ujenzi wake umekamilika kwa asilimia 100. Jengo hilo lilifunguliwa na Makamu wa Rais Mhe. Dk Philip Isdor Mpango, Septemba 13, 2022.
Pia, Serikali kupitia TBA imekamilisha ujenzi wa jengo la wagonjwa wa dharura na jengo la wagonjwa mahututi katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Katavi na ujenzi wa jengo la upasuaji, vifaa tiba na wodi ya mama na mtoto katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mbeya.

Mradi wa ujenzi wa nyumba za makazi ya watumishi wa Umma katika eneo la Magomeni Kota jijini Dar es Salaam ambapo majengo mawili tayari yameshakamilika na kuanza kutumika, majengo mengine mawili yakiwa kwenye hatua ya ujenzi.
Kadhalika, Serikali imefanikiwa kutekeleza mradi wa ujenzi wa jengo la ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya ambalo liliwekwa jiwe la msingi na Rais Dk Samia Suluhu Hassan Agosti 05, 2022 sasa umekamilika na kuanza kutumika.
Mradi mwingine ni pamoja na mradi wa ujenzi wa jengo la ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Mkalama ambalo lilifunguliwa na Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa Julai 17, 2022.
Ujenzi wa nyumba za makazi za viongozi wakuu wastaafu
Serikali kupitia TBA imefanikiwa kukamilisha mradi wa ujenzi wa nyumba za viongozi wastaafu ambapo mnamo Mei, 2021 Rais Dk Samia alimkabidhi nyumba ya kuishi Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Dk Jakaya Mrisho Kikwete iliyojengwa katika Wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam.
Pia, Serikali imefanikiwa kutekeleza mradi wa ujenzi wa nyumba ya Rais wa awamu ya Tano Hayati Dkt. John Pombe Magufuli ambapo Novemba 5, 2023 Rais Dk Samia alimkabidhi nyumba hiyo mjane wa Hayati Dk Magufuli Jijini Dar es Salaam. Nyumba hizo zimejengwa na Serikali kupitia TBA ambayo ilikuwa Mkandarasi na Mshauri Elekezi ikiwa ni utekelezaji wa kifungu namba 12 cha Sheria ya mafao ya hitimisho la kazi kwa viongozi wa siasa.
Katika kutekeleza majukumu yake, TBA imefanikiwa kuendelea kutekeleza malengo iliyojiwekea kwenye Mpango Mkakati wake wa Mwaka 2021/22- 2025/26, Dira ya Maendeleo 2025, utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya Mwaka 2020/25 chini ya Kifungu cha 55 ((h) (i-vii)) pamoja na Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs).
Hii inatokana na usimamizi thabiti wa viongozi wanaoteuliwa kuongoza Wizara ya Ujenzi pamoja na Menejimenti ya Wizara kwa ujumla. Pia viongozi wa Wizara wameendelea kutoa ushirikiano na miongozo mbalimbali ambayo imepelekea TBA kufikia mafanikio hayo.