
MAJERAHA yamekiweka rehani kibarua cha staa wa zamani wa Yanga, Yacouba Sogne baada ya upasuaji wa goti nchini Morocco kukamilika kwani amesema anakwenda kwao Burkina Faso ili kujiuguza na atakuwa nje ya uwanja msimu huu.
Yacouba ambaye alitua Tabora United msimu huu akitokea AS Arta Solar ya Djibouti, alisaini mkataba wa mwaka mmoja Tabora ambao unakwisha baada ya miezi miwili ijayo akiwa tayari ameshakosa mechi 10.
Akizungumza na Mwanaspoti kwa njia ya simu, Yaccouba alisema ametoka hospitali na sasa anafanya mazoezi ya kutembea taratibu akiwa chini ya uangalizi wa madaktari.
“Bado nina maumivu makali, lakini sitaweza kurejea tena msimu huu kwa kuwa nikitoka Morocco nitakwenda kwetu kujiuguza,” alisema mchezaji huyo.
Huenda rekodi ya majeraha ikakiweka matatani kibarua cha Yacouba kwani ndiye mchezaji ghali Tabora United, lakini mchango wake umekuwa mdogo kutokana na kuwa nje ya uwanja kwa muda mrefu.
Hata hivyo, hii sio mara ya kwanza kumtokea itakumbukwa kwamba hata Yanga ilimuacha kutokana na sababu kama hizo za majeraha ya muda mrefu.
Endapo atashindwa kumalizia msimu huu atakuwa amefanikiwa kuichezea Tabora United katika mechi 13 akikosa 17, amefunga mabao manne tangu alipoumia Novemba 29, 2024 kwenye mchezo wa ugenini dhidi ya KMC ambao alifunga bao la kwanza dakika ya 41 kwenye mechi hiyo waliyoshinda mabao 2-0 katika Uwanja wa KMC Complex.
Kikosi hicho kimesaliwa na michezo saba mkononi kumaliza Ligi Kuu Bara.
Ndani ya mechi 14 alizocheza Yacouba akiwa Tabora United amefunga mabao manne, huku kikosi hicho kikiweka rekodi ya kushika nafasi ya tano katika msimamo wa ligi kikiwa kimecheza michezo 23.
Awali, Mwanaspoti liliripoti kuwa baada ya kupata majeraha, Yacouba alirudi Dar es Salaam kwa ajili ya matibabu yaliyochukua takriban miezi mitatu, lakini alipoanza kupona na kuanza mazoezi bahati mbaya alijitonesha tena jeraha na vipimo vilionyesha ili apone ni vyema afanyiwe upasuaji huo wa ‘ligament’ na ndipo aliposafiri kwenda Morocco kwa daktari bingwa wa matatizo hayo.