
Dar es Salaam. Wakati mauzo ya mifugo katika masoko yaliyosajiliwa yakiongezeka kwa mwaka 2024, wadau wametaka wafugaji wapewe mbinu bora za ufugaji na mbegu ili kuongeza thamani ya mifugo yao.
Ripoti ya uchumi wa Kanda ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) inaonyesha kuwapo kwa ongezeko kubwa la mifugo inayouzwa kuliko fedha zinazopatikana robo ya mwaka iliyoishia Septemba 2024, ikilinganishwa na kipindi kilichotangulia.
Takwimu hizi zinaonyesha kuwa katika kipindi husika, idadi ya ng’ombe zilizouzwa ilifikia 929,114 kutoka ng’ombe 732,836 waliouzwa katika mwaka ulioishia Septemba 2023, huku thamani yake ikifikia Sh629,811 kutoka Sh504,836.2.
Ongezeko la idadi ya ng’ombe lilikuwa sawa na asilimia 26.78, huku thamani yake ikiongezeka kwa asilimia 24.75.
Mbuzi thamani yake ilifikia Sh56.83 bilioni kutoka Sh52.02 bilioni, huku idadi ya mbuzi zilizouzwa ikiwa 607,478 kutoka 436,326.
Kiasi kilichopatikana katika mauzo ya mbuzi ni ongezeko la asilimia 9.23, huku mifugo iliyouzwa ikiongezeka kwa asilimia 39.22. Katika kipindi hicho, kondoo waliouzwa walikuwa 269,902, ikiwa ni ongezeko kutoka kondoo 181,609 waliouzwa Septemba 2023, huku thamani yake ikifikia Sh24.42 bilioni kutoka Sh11.32 bilioni, mtawaliwa.
Akizungumzia suala hili, Mtaalamu wa Uchumi na Biashara, Dk Donath Olomi alisema mifugo mingi bado inatunzwa kienyeji bila kutumia mbinu bora za ufugaji, jambo ambalo linafanya tija yake kuwa ndogo.
“Kama ng’ombe anatumia muda mwingi kukomaa na hata akiuzwa hapati bei nzuri kwa sababu hana nyama nyingi na kilo ni chache, kinachotakiwa ni kuhakikisha mbegu zilizoboreshwa zinazalishwa kwa wingi watu wanafundishwa jinsi ya kuwatunza, malisho na kufanya mambo yao kibiashara,” alisema.
Alisema anatambua uwepo wa jitihada mbalimbali za kuingiza mbegu za kisasa sokoni, lakini jambo hilo linafanyika kwa kiwango kidogo, huku akieleza kuwa juhudi zaidi zinahitajika ili kuhakikisha wafugaji wanaweza kufuga zaidi, kupata kipato zaidi.
“Hili likifanikiwa linaweza kusaidia hata sekta ya usindikaji katika mifugo,” alisema Dk Olomi.
Mmoja wa wauzaji wa mifugo katika mnada wa Pugu, Masanja Magando anasema bei zilizopo sokoni wakati mwingine zimekuwa si zile zinazowapa moyo wauzaji ikiliganishwa na bei ya jumla waliyonunuliwa.
“Kuna wakati mifugo inakuwa mingi sana mnadani, lakini bei yake ni ndogo, hii haikupi fedha nzuri na wakati mwingine unaweza kuwa unatafuta faida ya Sh100,000 pekee kwa ng’ombe ukilinganisha na gharama ulizotumia hadi kufika mnadani,” anasema.
Anasema bei za mifugo zimekuwa zikipanda na kushuka kulingana na mahitaji yaliyopo sokoni, huku akisema wengi wanaonunua ni wale wanaokwenda kuchinja na kuuza kwa bei za rejareja.
“Kuhusu nje ya nchi sina uhakika kwa sababu sisi tunauza tu hapa mnadani, nje ya nchi inapelekwa nyama ambayo imekidhi vigezo vinavyotakiwa,” anasema Magando.
Hili linasemwa wakati ambao bajeti ya mifugo na uvuvi inaonyesha kuwapo kwa ongezeko la mifugo katika mwaka 2023/2024, ambapo ng’ombe ni milioni 36.6 mwaka 2022/2023 hadi milioni 37.9, mbuzi kutoka milioni 26.6 hadi milioni 27.6, na kondoo kutoka milioni 9.1 hadi milioni 9.4.
Pia hadi kufikia Aprili, 2024, jumla ya ng’ombe 2,957,724 na mbuzi na kondoo 2,828,248, waliuzwa katika minada mbalimbali hapa nchini ikilinganishwa na ng’ombe 2,218,293 na mbuzi na kondoo 2,121,187 waliouzwa katika mwaka 2022/2023.
Ongezeko la idadi ya mifugo iliyouzwa minadani limetokana na kuongezeka kwa mahitaji ya nyama katika soko la ndani na nje ya nchi pamoja na hamasa ya uvunaji wa mifugo. Mauzo hayo ya mifugo yalienda sambamba na ongezeko la uzalishaji wa nyama kutoka tani 803,264.3 mwaka 2022/2023 hadi tani 963,856.55 mwaka 2023/2024, ikiwa ni sawa na ongezeko la asimilia 16.7.
Kati ya hizo, nyama ya ng’ombe zilikuwa tani 612,808.50, mbuzi tani 134,403.35 na kondoo tani 28,290.