
Mtandao wa kijamii wa X, ambao zamani ulijulikana kama Twitter, umesimamisha akaunti ya lugha ya Kiebrania ya Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Seyyed Ali Khamenei.
Ujumbe kwenye akaunti hiyo ulisema kuwa imesimamishwa kwa madai ya kukiuka sheria za X.
Hatua hiyo imekuja saa chache baada ya akaunti hiyo kutuma ujumbe unaosema, “Utawala wa Kizayuni ulifanya makossa. Ulikosoea katika mahesabu yake kuhusu Iran. Tutaufanya uelewe nguvu, uwezo, ubinifu na irada ya taifa la Iran.”
Ujumbe huo ulifuatia shambulio la kigaidi la Israel dhidi ya Iran huku utawala huo ukiendeleza vita vya mauaji ya kimbari dhidi ya Ukanda wa Gaza na Lebanon.
Jukwaa la X linamilikiwa na Elon Musk, ambaye anaunga mkono utawala ghasibu wa Israel. Hii si mara ya kwanza mashirika ya Kimarekani kufunga akaunti za mitandao ya kijamii zinazofungamana na Ayatullah Khamenei.
Mnamo Februari, akaunti za Facebook na Instagram za Ayatullah Khamenei ziliondolewa na Meta, kampuni ya Kimarekani inayoendesha na kumiliki majukwaa hayo mawili.
Akaunti hizo zilifungua kufuatia mashinikizo ya makundi ya Kizayuni yanayounga mkono Israel ambayo yana ushawishi mkubwa Marekani.
Tangu Oktoba 7, 2023, Israel ilipoanzisha vita vya mauaji ya kimbari dhidi ya Ukanda wa Gaza, Meta imelenga na kuondoa kila maudhui inayoiunga mkono Palestina kwenye majukwaa yake ya Instagram na Facebook.
Katika upande wa pili X, Instagram na Facebook zimejiepusha kuchukua hatua dhidi ya akaunti zozote zinazomilikiwa na maafisa wa Israel ambao wamekuwa wakichochea mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina.