
Moshi. Sifael Shuma (92), aliyekuwa mmoja mwa vijana wanne walioshiriki tukio la kuchanganya udongo siku ya Muungano wa Tanganyika na Zanziba mwaka 1964 amefariki dunia.
Katika uhai wake, Shuma alitamani kuona muundo wa Muungano unakuwa wa nchi moja.
Hoja ya mama Shuma aliyefariki dunia Februari 20, 2025 katika Hospitali ya Mzena jijini Dar es Salaam, ndoto yake haikuwa mbali sana na Watanzania waliotaka Muungano unaozaa nchi moja au unaozaa Serikali tatu.
Ugumu wa hoja ya muundo wa Muungano, uliikumba pia Tume ya Mabadiliko ya Katiba chini ya Jaji Joseph Warioba mwaka 2013, huku baadhi wakitaka Serikali moja, wengine mbili na wengine ya mkataba.
Lakini wengi waliotoa maoni yao mbele ya tume walipendekeza muundo wa Serikali tatu na wachache walitaka muungano uvunjwe na kurudi kuwa na nchi ya Tanganyika na ile ya Zanzibar.
Mama Shuma aliyetamani kuona muundo wa Serikali moja au wale waliotaka muundo wa Serikali tatu kwa maana ya Tanganyika, Zanzibar na ile ya Shirikisho, walikuwa na dhamira ya kutaka uwepo wa muungano imara.
Leo Watanzania wanapoomboleza msiba wa mama Shuma ambaye Jumatano ya Februari 26, 2025 mwili wake utapumzishwa katika nyumba yake ya milele, bado maoni yake, ndoto zake na wosia wake unajadilika.
Kwa mujibu wa ratiba ya mazishi, kesho Jumanne ya Februari 25, 2025 mwili wake utachukuliwa kutoka Hospitali ya Lugalo na kupelekwa nyumbani kwake ambako kutakuwa na ibada ya kumuaga katika usharika wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Makongo jijini Dar es Salaam.
Kesho saa 6:30 mchana, safari ya kuelekea nyumbani alikozaliwa huko Machame Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro itaanza na siku inayofuata kutafanyika ibada ya maziko na baadaye kupumzishwa katika nyumba yake ya milele.
Mama Shuma ambaye ndiye alikuwa amebaki hai, kifo chake kimefunga ukurasa wa vijana wanne, wawili kutoka Zanzibar na wawili kutoka Tanganyika walioshiriki tukio la kuchanganya udongo, ikiwa ni ishara ya Muungano wa nchi hizo mbili.
Vijana wengine walioshiriki tukio na wametangulia mbele ya haki wakiwa tayari watu wazima ni Hassan Omar Mzee (76) na Khadija Abbas Rashid (74) (wote kutoka Zanzibar) na Hassaniel Mrema (80) na sasa Shuma waliotoka Tanganyika.
Mzee na Mrema ndio walioshiriki kushika chungu kilichowekwa udongo wa nchi hizo mbili, Khadija na Shuma walibeba vibuyu vilivyokuwa na udongo. Shuma alibeba kibuyu chenye udongo wa Tanganyika na Khadija wa Zanzibar.
Udongo wa Tanganyika ulitoka wapi
Katika mahojiano maalumu na Mwananchi Aprili 2006 huko Machame, mkoani Kilimanjaro ikiwa ni sehemu ya makala za toleo maalumu la maadhimisho ya Muungano, Shuma aliyezaliwa mwaka 1934 huko Machame, alieleza ndiye aliyepewa dhamana ya kusafiri na kibuyu kilichokuwa na udongo wa Tanganyika hadi Dar es Salaam miaka 60 iliyopita.
Katika mahojiano hayo, alisema mwaka 1964 aliteuliwa na kamati kuu ya Halmashauri Kuu ya TANU Mkoa wa Kilimanjaro, kuupeleka udongo uliochanganywa na wa Zanzibar na kuzaa muungano ambao ni fahari ya Tanzania.
“Sifahamu ni vigezo gani vilitumika kuniteua mimi kati ya mamilioni ya Watanzania wakati huo, najiona kama mtu niliyethaminiwa sana na Serikali ya TANU wakati huo,”alieleza mama Shuma katika mahojiano hayo.
Alisema aliondoka Moshi na Kibuyu kilichokuwa na udongo huo hadi Dar es Salaam na kukutana na mwenzake wa Zanzibar na walifanya mazoezi kwa siku nne namna watakavyoshika vibuyu hivyo.
“Kwa kweli tangu siku ile sijawahi kumuona tena mwenzangu yule wa Zanzibar wala simkumbuki jina kwa sababu tulionana siku chache sana tena katika hekaheka nyingi.”
“Wakati nakabidhiwa kibuyu kile niliambiwa kuwa, udongo ule ulikuwa umechukuliwa Mlima Kilimanjaro na hii nadhani ilitokana na umashuhuri wa mlima wenyewe ambao kila Mtanzania anajivunia nao,” alisema Shuma.
Alieleza kuwa, anakumbuka tendo la kuchanganywa udongo lilifanywa na Mwalimu Julius Nyerere aliyekuwa Rais wa Tanganyika huru na Rais Abeid Aman Karume aliyekuwa Rais wa visiwa vya Zanzibar .
“Nakumbuka pia alikuwepo mzee Kawawa (Rashid) na Mangi Mkuu (hakumkumbuka vizuri jina) ambaye alifanya kama vile tambiko la jadi kwa kumvisha mwalimu (Nyerere) koti la ngozi kama heshima ya mtawala,”alisema mama Shuma.
“Sherehe zile zilikuwa ni kubwa,” alisema mama Shuma na kuongeza kuwa hata miaka iliyofuata tukio lile lilikuwa likikumbukwa kwa namna ya pekee na sherehe zilikuwa zikimgusa kila Mtanzania popote pale alipokuwa.
Shamrashamra za Muungano zimepoa
Katika mahojiano hayo, alieleza sasa kumbukumbu ya tendo lile japo inaadhimishwa kitaifa lakini haina shamrashamra na hamasa kama ilivyokuwa katika uongozi wa awamu ya kwanza chini ya Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere.
“Wakati ule mpaka maduka yalikuwa yakifungwa na watu wote wanahamasika kwenda kwenye maadhimisho ya kumbukumbu ya tendo lile kila mwaka lakini sasa mambo ni tofauti ni tukio ambalo halina msisimko tena kama zamani,” alisema.
Alisema anaamini malengo ya Muungano ni mazuri japo kwa mtazamo wake kuna mambo ambayo yanaufanya upoteze ile sifa ya kulifanya Taifa la Tanzania kuwa nchi moja baada ya Muungano wa Tangayika na Zanzibar.
Alivyotamani Serikali moja
Moja ya mambo ambayo mama Shuma aliyaona yanatia doa Muungano ni ile hali ya kuwepo kwa Serikali mbili kwa maana ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) licha ya nchi mbili kuungana.
“Kama kweli ni nchi mbili zimeungana mimi nadhani na Watanzania walio wengi wanaliona hilo, tulitegemea tungekuwa na Rais mmoja lakini kuwa na marais wawili katika nchi moja imepoteza kabisa dhana ya Muungano,” alieleza.
Kwa mtazamo wake, katika uchaguzi, Watanzania wangekuwa wanampigia kura Rais mmoja wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kisha makamu wawili wa Rais mmoja wa Tanzania Bara na mwingine wa Zanzibar.
Alieleza hali hiyo ndiyo inayotoa picha kwamba Tanzania ni nchi moja lakini yenye marais wawili na wananchi wao wakiwa na mtazamo na hulka tofauti hali inayotoa mwanya wa kuwepo kwa tabaka la uzanzibari na ubara.
Kwa mujibu wa mama Shuma, Muungano wa nchi hizi mbili ni mzuri isipokuwa unaonekana kuwa na mushkeli kutokana na dosari za hapa na pale alizosema kama zitarekebishwa zitaufanya Muungano uwe imara.
“Kama sasa tumefikia hatua ya kuunganisha nchi zetu za Afrika Mashariki itakuwa ni kichekesho cha karne kufikiria kuvunja Muungano. kinachotakiwa turekebishe dosari na manung’uniko ya Muungano,” alisisitiza mama Shuma.
Alieleza binafsi anawachukuliwa watu wanaotaka kuvunja Muungano kama wabinafsi ambao hawaitakii mema Tanzania ambayo imeendelea kuwa kisiwa cha amani na utulivu katika bara la Afrika na duniani kote.
Mama Shuma ni nani?
Mama Shuma aliyezaliwa mwaka 1934, alipata elimu yake Shule ya Msingi Mkwarungo na baadaye Shule ya wasichana ya Machame kisha alijiunga na Sekondari ya Wasichana Tabora na kuhitimu kidato cha nne.
Alijiunga na Chuo cha Ualimu Loleza mkoani Mbeya mwaka 1957 na baadaye wakahamia Chuo cha Ualimu Mpwawa.
Baada ya kuhitimu mwaka 1959 alipangiwa kuwa mwalimu Shule ya Sekondari Machame iliyopo Wilaya ya Hai.
Mwaka 1962 na 1963 alikwenda kusoma Chuo Kikuu cha Southampton cha nchini Uingereza.
Huko alisomea elimu na hesabu na baada ya kumaliza alirejea tena Machame Sekondari na kupewa umakamu mkuu wa shule.
Kutokana na utendaji kazi wake mzuri na wenye ufanisi mkubwa, mama Shuma alipewa madaraka kamili ya kuwa mkuu wa Shule ya Machame mwaka 1970 wadhifa aliodumu nao hadi alipostaafu mwaka 1993.
Hakuna ubishi wa mawazo yake, dosari za Muungano ndiyo zimejikita kwa Watanzania wengi, lakini leo hayupo tena duniani, ingawa yale aliyoyatamani kama njia ya kuimarisha Muungano yanabaki kama wosia.
Mahojiano maalumu na mama Shuma yalifanywa na Daniel Mjema, Aprili 16, 2006 na kuchapishwa katika Gazeti la Mwananchi la Aprili 26, 2006, na leo tumerejea maono, fikra na wosia wake huo kwa Watanzania.