
Dar es Salaam. Kampuni ya Serengeti Breweries Limited (SBL) imemtangaza Jacqueline Woiso kama mjumbe wake wa bodi, kuanzia Januari 10, 2025.
Kabla ya kutangazwa kuwa mjumbe wa bodi ya kampuni hiyo kubwa ya vileo nchini Woiso amefanya kazi katika ngazi ya kiongozi kwa zaidi ya miaka 20 katika mashirika ya kimataifa na ya ndani kwenye sekta za benki na vyombo vya habari.
Woiso amehudumu katika nafasi Mkurugenzi Mtendaji kwa zaidi ya miaka saba, na hivyo kuleta utaalamu mkubwa katika uongozi wa kimkakati, fedha za kampuni, usimamizi wa rasilimali, mahusiano ya umma, na utayarishaji wa sera.
Kwa sasa Woiso ni Mkurugenzi Mtendaji wa MultiChoice Tanzania (DSTv), nafasi aliyoishika tangu Novemba 2018. Katika uzoefu wake wa miaka 19 katika sekta ya benki, alifanya kazi na taasisi maarufu kama vile Standard Chartered Bank, Barclays Bank, na Bank M nchini Tanzania.
Mbali na mafanikio yake ya kiutendaji, Woiso ni mtaalamu mwenye uzoefu katika bodi mbalimbali na amechangia ukuaji na uongozi bora wa taasisi za umma na binafsi kwenye sekta kama vile benki, afya, elimu, utamaduni, sanaa, na utalii kwa zaidi ya miaka kumi.
Kielimu Woiso ana Shahada ya Uzamili ya Utawala wa Biashara kutoka Milpark Business School, Afrika Kusini, Stashahada ya Juu ya Utawala wa Biashara kutoka Chuo cha Institute of Development Management, Mzumbe, na Cheti cha Ukurugenzi kutoka Institute of Directors Tanzania.
Kadhalika Woiso ni mwanachama wa The Boardroom Africa, akionesha zaidi kujitolea kwake katika masuala ya uongozi.
Katika taarifa ya kumtangaza Woiso Mwenyekiti wa Bodi wa SBL Paul Makanza inasema bodi ina imani na uzoefu wake mkubwa, maarifa yake ya kimkakati, na shauku yake ya ukuaji na uongozi bora wa kampuni vitatoa mchango mkubwa katika kuendeleza dira na ajenda ya ukuaji wa SBL.
“Tunamkaribisha sana Jacqueline Woiso ndani ya Serengeti Breweries Limited na tunatazamia safari yake yenye matokeo chanya pamoja nasi,” amesema Makanza.