Wizi wa mtandaoni waliza Watanzania Sh5.3 bilioni

Dar es Salaam. Tanzania imepoteza Sh5.345 bilioni kutokana na udanganyifu mwaka 2024, matukio yanayohusishwa na udanganyifu huo ni uhamishaji wa fedha kupitia simu za mkononi, benki, na utoaji wa fedha kwa ATM, kama inavyoonyeshwa na ripoti mpya ya Takwimu za Uhalifu na Ajali za Barabarani.

Kiasi hicho kinaashiria ongezeko kutoka Sh5.067 bilioni zilizoripotiwa mwaka uliopita, jambo linaloonyesha kuongezeka kwa mienendo ya udanganyifu wa kifedha kwa njia ya mtandao.

Taarifa hiyo inakuja wakati ambapo Watanzania wamekuwa wakilalamikia kutapeliwa kwa njia ya mitandao ya simu, wakitumiwa ujumbe wa maandishi wakitakiwa kutuma ‘fedha kwa namba hii’.

Jumbe hizo, ambazo hutumwa kupitia namba ya simu, huomba fedha kwa ajili ya kodi ya nyumba, ada ya watoto, gharama za matibabu ya mgonjwa aliyepo hospitalini, au michango ya harusi.

Ripoti hiyo ya Jeshi la Polisi Tanzania, iliyotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), imetaja sababu za ongezeko la matukio hayo kuwa ni hali ngumu ya kiuchumi, ukosefu wa ajira kwa vijana, utandawazi, na tamaa ya kupata fedha kwa njia za haraka na zisizo halali.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, matukio 4,091 ya uhalifu unaohusiana na udanganyifu wa kifedha yaliripotiwa mwaka jana, ikilinganishwa na matukio 3,731 mwaka uliotangulia.

Hali hiyo inaonyesha ongezeko la matukio 360, sawa na asilimia 9.6. Hata hivyo, ni Sh254.1 milioni pekee ndizo zilizopatikana katika kipindi hicho.

Miongoni mwa matukio yaliyoripotiwa, 3,460 yalihusiana na miamala ya simu za mkononi, yakifuatiwa na matukio 457 ya kuhamisha fedha kupitia benki.

Pia, udanganyifu uliohusisha mashine za kutolea fedha (ATM) ulikuwa na matukio machache zaidi, yakibainika kuwa 74 pekee, huku aina nyingine za udanganyifu wa kifedha zikichangia kesi 100.

Ripoti hiyo inataja Mkoa wa Ilala kuwa ndiyo umeathirika zaidi, ukirekodi hasara ya zaidi ya Sh1.602 bilioni kutokana na udanganyifu wa miamala ya simu.

Watu 465 walikamatwa kuhusiana na uhalifu huo, wakiwemo wanaume 367 na wanawake 98, ikiwa ni juhudi za kukabiliana na matukio hayo.

“Askari polisi wanapaswa kuendelea kupatiwa mafunzo kuhusu mbinu na teknolojia za kisasa ili kuwazidi maarifa wahalifu wanaotumia mbinu mpya zinazoletwa na maendeleo ya sayansi na teknolojia,” ripoti imesisitiza.

Ripoti hiyo imekuja wakati ambapo takwimu kutoka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) zinaonyesha asilimia 33 ya matukio ya wizi wa fedha kwenye mitandao yalitokea kati ya Desemba 2024 hadi Machi 2025.

Wilaya ya Kilombero ilirekodi kiwango kikubwa cha matukio, huku mtoa huduma wa mawasiliano Airtel akiongoza kwa idadi kubwa ya majaribio ya udanganyifu—yakifikia matukio 5,876—ikifuatwa na TTCL (3,925), Vodacom (3,143), Yas (2,484), na Halotel kwa matukio 1,724.

Akizungumza katika hafla ya hivi karibuni, Kamishna wa Polisi wa Idara ya Upelelezi wa Kisayansi, Shaban Hiki, alisema kasi ya maendeleo ya kiteknolojia imeifanya kuwa vigumu kudhibiti uhalifu unaohusiana na mtandao.

“Upanuzi wa majukwaa ya kidijitali umeleta fursa nyingi, lakini pia umetufunulia mifumo ya uhalifu ya kisasa.

“Ili kushughulikia hili, Serikali na wadau wanapaswa kuwekeza katika teknolojia ya kisasa na kupitia sheria zilizopo ili kuhakikisha zinakidhi mahitaji ya wakati huu.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *