Wizara yatoa angalizo matumizi ya plastiki

Unguja. Waziri wa Afya, Nassor Ahmed Mazrui amesema matumizi ya vyombo vya plastiki yana madhara ya kiafya katika mwili wa binadamu hasa vinapotumika vibaya na kwa muda mrefu.

Mazrui amesema hayo leo Jumanne Februari 18, 2025 katika Mkutano wa 18 wa Baraza la Wawakilishi, alipojibu swali la mwakilishi wa Kwerekwe, Ameir Abdalla Ameir.

Ameir alitaka kufahamu madhara ya kiafya yanayotokana na matumizi ya vyombo vya plastiki.

Waziri Mazrui amesema sababu kuu za madhara hayo kwa mujibu wa wataalamu ni kuvuja kwa kemikali kwenye chakula au kinywaji hasa wakati vyombo hivyo vinapopashwa moto au vinapotumiwa kwa chakula chenye mafuta mengi au tindikali.

“Uharibifu wa afya kupitia chembechembe ndogo za plastiki (microplastics), utafiti unaonyesha plastiki huweza kuoza na kutoa chembechembe ndogo zinazoingia mwilini kupitia chakula na maji,” amesema Mazrui pasipo kutaja utafiti huo.

Amesema athari za kiafya zinazoweza kusababishwa na utumiaji wa vyombo vya plastiki ni pamoja na matatizo ya homoni, uzazi, saratani na magonjwa ya moyo.

Magonjwa mengine ni kuathiri mfumo wa homoni na maendeleo ya watoto na husababisha matatizo ya uzazi kwa wanaume na wanawake.

Hata hivyo, ametoa njia ambazo zinaweza kusaidia kuepuka madhara ya vyombo vya plastiki ikiwamo kuepuka kupasha chakula kwenye plastiki badala yake watu watumie vyombo vya kioo, chuma au udongo.

Vilevile, kuchagua plastiki zilizo na alama ya BPA-Free, kutumia chupa za glasi au chuma cha pua badala ya plastiki na kuepuka plastiki za matumizi ya mara moja.