Wizara yajipanga kuongeza idadi ya watalii, kuboresha vivutio

Wizara yajipanga kuongeza idadi ya watalii, kuboresha vivutio

Unguja. Wizara ya Utalii na Mambo ya Kale imepanga kutekeleza vipaumbele 10, vikiwemo kuimarisha vivutio vya utalii vilivyopo nchini kwa lengo la kuongeza idadi ya wageni wanaotembelea visiwa vya Zanzibar.

Akisoma hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2025/2026, katika Baraza la Wawakilishi, Kaimu Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale, Tabia Maulid Mwita amesema hatua hiyo inalenga kuboresha sekta ya utalii ambayo ni miongoni mwa nguzo kuu za uchumi wa Zanzibar.

“Kipaumbele chetu ni kuongeza idadi ya watalii kutoka nje ya nchi kwa kuimarisha vivutio vya utalii vilivyopo, na pia kuanzisha maeneo mapya yenye mvuto wa kiutalii,” amesema Waziri Tabia.

Aidha, amesema wizara inaendelea na jitihada za kuwahamasisha wawekezaji kuwekeza katika maeneo ya urithi wa kihistoria na mambo ya kale, kwa lengo la kuyarejesha katika hali yake ya awali na kuyatunza kwa ajili ya vizazi vijavyo.

“Tunataka maeneo haya yawe na hadhi inayostahili, yatumike kama darasa la kihistoria kwa vizazi vya sasa na vijavyo, sambamba na kuwa vivutio muhimu kwa watalii kutoka mataifa mbalimbali,” ameongeza.

Katika bajeti hiyo wizara imeliomba baraza hilo kuidhinishiwa Sh45.032 bilioni kwa ajili ya kutekeleza vipaumbele hivyo.

Pia, amesema wanataka kuendelea na mradi wa kuzifanyia matengenezo baadhi ya nyumba zilizopo katika hali mbaya ndani ya eneo la Mji Mkongwe.

Hata hivyo, licha ya wizara katika bajeti ya mwaka 2024/25 kuomba Sh9 bilioni kwa ajili ya ukarabati wa nyumba hizo, lakini hadi Machi mwaka huu hakuna fedha yoyote iliyoingizwa kwenye akaunti.

Amesema Mamlaka ya Hifadhi na Uendelezaji Mji Mkongwe ilifanya utafiti mdogo wa majengo yaliyopo ndani ya eneo hilo na kugundua majengo zaidi ya 160 yapo katika hali mbaya, na kati ya hayo 36 hali yake ni mbaya zaidi.

 “Katika jitihada za kutatua changamoto za majengo hatarishi yaliyopo ndani ya eneo la Mji Mkongwe, Wizara iliwasilisha mradi huu katika mwaka wa fedha 2024/25 wa ukarabati wa majengo 10 na kutengewa bajeti ya Sh9 bilioni na hadi kufikia Machi 2025.

“Mradi huu bado haujaingiziwa fedha za malipo kwa makandarasi, licha ya utekelezaji wa mradi huu kwa baadhi ya majengo ukiendelea, Wizara imeanza kuyafanyia matengenezo makubwa majengo manne,” amesema.

 Kipaumbele kingine ni kuendelea kukiimarisha kikosi cha Polisi Utalii ili kutoa huduma bora na kuendelea kuwashawishi wawekezaji kuwekeza katika maeneo ya urithi wa kihistoria na Mambo ya Kale, ili yarudi  katika uasili wake na kutunza historia kwa faida ya vizazi vijavyo.

Kukamilisha mapitio ya sera ya utalii pamoja na mpango kazi wa utekelezaji ikiwemo uzinduzi wa sera ya makumbusho na urithi wa mambo ya kale na kukamilisha mapitio ya sheria ya utalii ya mwaka 2009, na marekebisho yake ya mwaka 2012.

Kingine ni kukamilisha mapitio ya sheria ya uanzishwaji wa Mamlaka ya Makumbusho na Urithi wa Mambo ya Kale, na kukamilisha utekelezaji wa mapendekezo ya utafiti uliofanywa kitaifa wa uhimilivu wa sekta ya utalii Zanzibar.

Ongezeko watalii

Waziri Tabia amesema kutokana na jitihada zinazofanywa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar za kuitangaza Zanzibar kiutalii ndani na nje ya nchi, kumekuwa na ongezeko kubwa la watalii wanaoingia nchini kwa mwaka, kutoka 260,644 mwaka 2020 hadi kufikia watalii 737,775 mwaka 2024 ambalo  ni sawa na asilimia 65.

Amesema Kamisheni ya Utalii kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imeendelea kuchukua hatua ya kuvitangaza vivutio vya utalii vya Zanzibar ndani na nje ya nchi.

Kwa mujibu wa wizara, jitihada hizo zimewezesha kuongezeka kwa idadi ya watalii walioingia hapa nchini mwaka 2024 ambapo idadi ya watalii walioingia nchini iliongezeka kwa asilimia 15 kutoka watalii 638,498 mwaka 2023 hadi kufikia watalii 736,755 mwaka 2024.

Kutokana na juhudi hizi, uwekezaji katika sekta ya utalii umeongezeka kutoka miradi ya kitalii 995 iliyosajiliwa katika mwaka 2020 hadi kufikia miradi 1,695 sawa na ongezeko la asilimia 70.4 katika mwaka 2024.

Miradi hii inamilikiwa na wazalendo, wageni au ubia baina ya wazalendo na wageni. Miradi husika ni mahoteli, mikahawa na miradi ya mawakala wa utalii.

Amesema idara imepokea jumla ya wageni 37,036 waliotembelea katika maeneo mbalimbali ya kihistoria ambapo kati ya hao 23,418 walitoka nje ya Tanzania, 2,393 walikuwa ni Watanzania, wageni maalumu wa kiserikali ni 45 na wanafunzi kutoka shule mbalimbali walikuwa 11,180.

Kulinda watalii

Kwa kushirikiana na kikosi cha Polisi Utalii na Diplomasia, maofisa wa Kamisheni ya Utalii wamefanya doria maalumu na za kawaida katika maeneo mbalimbali ya utalii nchini, pamoja na kusimamia utoaji huduma za utalii kwa wageni wanaotumia magari ya kubebea watalii.

“Hadi kufikia Machi, 2025, jumla ya doria 620 zimefanyika katika maeneo ya Kizimkazi, Jambiani, Paje, Bwejuu, Michamvi, Unguja Ukuu na Uroa kwa Mkoa wa Kusini Unguja, pamoja na maeneo ya Matemwe, Kiwengwa, Nungwi, Pwani Mchangani na Kendwa kwa Mkoa wa Kaskazini Unguja na maeneo yote ya utalii kwa Mkoa wa Mjini Magharibi,” amesema.

Akiwasilisha maoni ya kamati  Said Saleh Salim amesema licha ya ukusanyaji mzuri wa mapato ya wizara kwa asilimia 96, kamati imebaini kuwa imepokea fedha ndogo za matumizi mengineyo katika idara zake kwa kipindi cha Julai 2024 hadi kufikia Machi 2025, jambo linalosababisha kusuasua kwa utekelezaji wa programu za idara pamoja na miradi ya maendeleo.

“Kamati inaishauri wizara katika bajeti ya 2025/26 kushirikiana na sekta binafsi katika uwekezaji wa maeneo ya kihistoria kwa lengo la kuyaendeleza maeneo hayo, ambayo yataleta tija kubwa ikiwa yataendelezwa,” amesema.

Pia, kwa upande wa Serikali kuendelea kutafuta wafadhili mbalimbali wa kusaidia uendelezaji wa miradi ya kitalii kama vile mwekezaji wa sasa katika miradi ya Mji Mkongwe ambaye ni kampuni ya Infinity Foundation, inayotekeleza miradi ya maeneo ya Mji Mkongwe kwa ufanisi mkubwa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *