
Unguja. Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi imeweka mkazo katika utekelezaji wa vipaumbele vyake vinavyolenga kuendeleza miundombinu ya barabara, bandari na viwanja vya ndege, sambamba na kuimarisha Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama), ili kuiwezesha Zanzibar kufikia uchumi wa kidijitali.
Akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya bajeti ya mwaka 2025/2026 leo, Mei 22, 2025, Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Dk Khalid Salum Mohamed, amelomba Baraza la Wawakilishi kuidhinisha jumla ya Sh1.589 trilioni kwa ajili ya kutekeleza mipango ya wizara hiyo.
Amesema miongoni mwa miradi muhimu iliyoainishwa kwenye bajeti hiyo ni ujenzi wa mkonga wa kimataifa wa mawasiliano kupitia baharini, kutoka Mombasa (Kenya) hadi Micheweni (Pemba) na kuunganishwa na Fumba (Unguja), ambao umepangiwa kutumia Shilingi bilioni 30.
Pia, itaanza ujenzi wa kituo mbadala cha kuhifadhia taarifa katika maeneo ya uwekezaji Fumba ambao nao umepangiwa Sh30 bilioni.
“Tutaimarisha huduma za mtandao katika maeneo ya umma (Public Wi-Fi) zaidi katika maeneo ya Amani, Nyamanzi na Kijangwani,” amesema.
Amesema kazi nyingine ambazo idara ya Mawasiliano imepanga kutekeleza ni kutayarisha miongozo ya mageuzi ya kidijitali Zanzibar pamoja na kukamilisha sheria ya ulinzi wa taarifa binafsi na faragha (PDPC) na wabunifu chipukizi.
Waziri huyo alibainisha pia kuwa wizara itatekeleza miradi mingine muhimu ikiwemo ya ujenzi wa uwanja wa ndege wa Nungwi kwa gharama ya Sh2.5 bilioni, utakaotoa huduma kwa viwango vya kimataifa.
Vingine ni ujenzi wa bandari mpya ya kisasa ya abiria Maruhubi, kwa gharama ya Sh130 bilioni 130, ujenzi wa boti mbili za kisasa, kila moja ikiwa na uwezo wa kubeba abiria 650, zitakazofanya safari kati ya Unguja, Dar es Salaam na Pemba.
Amesema kwa sasa, Serikali haina chombo chake cha usafiri wa majini katika maeneo hayo, hali inayosababisha utegemezi kwa vyombo vya binafsi.
Vilevile, Serikali itaendelea na ujenzi wa Bandari Jumuishi ya Mangapwani na kuweka miundombinu ya msingi pamoja na kukamilisha nyumba za fidia kwa wakazi wa eneo hilo. Mradi huo umetengewa Sh205.1 bilioni.
Katika kuimarisha mfumo wa usafiri wa umma, wizara itafanya utafiti wa kina utakaosaidia kutoa mwelekeo sahihi wa maboresho ya sekta hiyo.
Kwa upande wake, Kamati ya Mawasiliano, Ardhi na Nishati kupitia Mwenyekiti wake, Yahya Rashid Abdulla, iliishauri Serikali kuuharakisha ukamilishaji wa matengenezo ya meli ya MV Mapinduzi II na kuipeleka chelezoni Mombasa kwa ukaguzi, ili irejee kazini na kupunguza changamoto za usafiri.
Pia, wameitaka Serikali kuzifanyia kazi changamoto za Bandari ya Malindi, hasa msongamano wa makontena katika bandari kavu ya Maruhubi, kuchelewesha utoaji wa mizigo, na uwepo wa makontena mengi yasiyo na mizigo.
Hata hivyo, kamati iliipongeza Serikali kwa juhudi za kujenga bandari kavu mpya yenye ukubwa wa hekta 3.05 katika eneo la Maruhubi, hatua itakayosaidia kupunguza mzigo katika Bandari ya Malindi na kuongeza ufanisi wa utoaji wa huduma.