Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imelaani vikali kitendo cha Israel cha kumuuwa kikatili mwanamke wa Kiirani na mumewe raia wa Lebanon huko Beirut.
Ismail Baqaei Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amelaani jinai mpya ya utawala wa Kizayuni ya kumuuwa kikatili Masoumeh Karbasi raia wa Iran na mumewe Mlebanoni Reza Awadheh, na kutoa mkono wa pole na pongezi kwa familia, kwa nchi mbili tukufu na kwa viongozi wa Iran na Lebanon kufuatia kuuawa shahidi kwa wanandoa hao wawili.

Baqaei ameashiria video iliyochapishwa ikionyesha namna Israel ililivyowauwa kigaidi mwanamke huyo raia wa Iran pamoja na mumewe katika eneo la kiraia na katika mtaa wenye shughuli nyingi, na kuitaja hujuma hiyo ya utawala wa Kizayuni kuwa ni mfano kamili wa ugaidi na jinai ya kivita.
Wakati huo huo ubalozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran mjini Beirut jana ulituma ujumbe katika ukurasa wa X kwamba: Mmoja wa wanawake wa Kiirani wanaoishi Lebanon, aitwaye Masoumeh Karbasi ameuawa shahidi pamoja na mumewe katika shambulio la kinyama la drini ya utawala wa Kizayuni juzi Jumamosi katika eneo la kiraia la Jounieh kaskazini mwa mji mkuu wa Lebanon, Beirut.
Msemaji huyo wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Iran amemuenzi mwanamama huyo Muirani aliyeuliwa shahidi ambaye pia alikuwa mwanaharakati wa vyombo vya habari anayeunga mkono Palestina na kusisitiza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran itatumia suhula zote zilizopo kufuatilia suala hilo na kuuwajibisha utawala wa Kizayuni kwa jinai zake.