Wizara ya Elimu Zanzibar imepiga marufuku uuzaji wa vyakula na vinywaji shuleni

Wizara ya Elimu Zanzibar imepiga marufuku uuzaji wa vyakula na vinywaji shuleni

Unguja. Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, imetoa katazo la uuzaji wa vyakula na vinywaji katika maeneo ya shule za Serikali na binafsi, ikiwa ni hatua ya tahadhari ya kulinda afya za watoto dhidi ya magonjwa ya mlipuko yanayoweza kusababishwa na mvua zinazoendelea kunyesha kisiwani Unguja.

Taarifa rasmi ya katazo hilo ilitolewa jana, Mei 19, 2025, na Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Khamis Abdulla Said, aliyesisitiza kuwa marufuku hiyo inalenga kuhakikisha usalama wa afya za wanafunzi katika kipindi hiki cha mvua, ambacho mara nyingi huambatana na ongezeko la magonjwa kama kipindupindu na kuhara.

“Tuna wajibu wa pamoja kuwalinda watoto wetu dhidi ya hatari zinazotokana na ulaji wa vyakula visivyo salama, hasa katika kipindi hiki ambacho mazingira yanakuwa na changamoto nyingi za kiafya,” ilisomeka sehemu ya taarifa hiyo.

Aidha, wizara imewaagiza walimu wakuu wa shule zote kuhakikisha usafi wa mazingira unazingatiwa na kwa ufuatiliaji wa karibu.

Vilevile, imetoa wito kwa wazazi na walezi kuchukua tahadhari zaidi na kuwahimiza watoto wao kuwa waangalifu wanapokwenda na kurudi shuleni.

Maoni ya wananchi

Baadhi ya wazazi na walezi wamepongeza hatua hiyo ya Serikali, wakisema ni muhimu kwa afya za watoto wao.

Madina Issa Ahmada, mkazi wa Tunguu, amesema marufuku hiyo itawasaidia watoto kuepuka maradhi, hasa yale ya mlipuko ambayo huenea kwa kasi kipindi cha mvua.

“Hili ni jambo jema. Wazazi tunapaswa kujenga utamaduni wa kuwapikia watoto wetu chakula cha nyumbani badala ya kuwategemea wauzaji wa vyakula mashuleni, ambao mara nyingi hupika katika mazingira yasiyo salama,” amesema Madina.

Kwa upande wake, Jokha Said Nassor, mkazi wa Bububu, ameunga mkono katazo hilo lakini akasisitiza umuhimu wa Serikali kufanya ufuatiliaji wa utekelezaji wake kwa karibu.

Wafanyabiashara wataka ufafanuzi

Wakati huohuo, baadhi ya wafanyabiashara wanaojihusisha na uuzaji wa vyakula na vinywaji karibu na shule wamesema wanahitaji ufafanuzi zaidi kutoka serikalini kuhusu aina ya bidhaa zilizokatazwa.

Juma Ahmada Ali, mmoja wa wauzaji wa bidhaa hizo, amesema:

“Ni muhimu kwa Serikali kubainisha wazi ni vyakula na vinywaji gani vimepigwa marufuku ili kuepuka mkanganyiko. Wengine tunauza maji ya chupa na matunda je, nayo ni marufuku?”amehoji Ali.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *