Wizara tano kushughulikia changamoto walimu wasio na ajira

Dodoma. Serikali imeunda timu ya wataalamu itakayoshirikisha wizara tano kwa ajili ya kushughulikia changamoto za Umoja wa Walimu Wasiokuwa na Ajira Tanzania  (Neto) kuanzia mwaka 2015 hadi mwaka 2023.

Timu hiyo itashirikisha Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, na Wizara ya Fedha.

Katibu Mkuu wa Neto, Daniel Mkinga, amesema hayo leo Alhamisi, Machi 13, 2025, walipozungumza na waandishi wa habari baada ya kukutana na mawaziri watatu.

Mawaziri waliokutana nao jana jijini Dodoma ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene; Waziri wa Tamisemi, Mohamed Mchengerwa na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda.

Amesema katika kikao chao hicho, kilichowashirikisha wawakilishi wa walimu hao kutoka mikoa mbalimbali nchini, waliwasilisha nakala ya taarifa yenye kurasa 22 juu ya changamoto wanazokutana nazo walimu wasio na ajira.

Amesema katika kikao hicho walizungumza kuhusu masuala mbalimbali, yakiwemo yanayohusiana na mitalaa, usaili, umri wa kustaafu, na namna ya uzalishaji wa walimu.

“Tulikubaliana kuunda timu ya wizara tano ambazo zitafuatilia changamoto tulizoziwasilisha. Waziri alituomba kuwa wavumilivu kwa kipindi cha siku 30 hadi 45, ambapo wizara zaidi ya tano zitakaa na kuunda timu ili kuzungumza mambo kadhaa ambayo tuliyaeleza,” amesema.

Kuhusu suala la walimu wa masomo ya uchumi kutopata nafasi ya kwenda katika usaili katika ajira zilizopita kutokana na mfumo wa ajira kukataa, Mkinga amesema changamoto hiyo ilitatuliwa papo hapo na Simbachawene na Profesa Mkenda.

Amesema sasa walimu hao waliosoma masomo ya uchumi watapata kibali cha kufanya usaili kwa nafasi za ajira zitakazotangazwa baadaye.

“Nawaomba Watanzania, wana-Neto na walimu wasiokuwa na ajira nchini, tusubirie siku 30 hadi 45, kwani zinaweza kuleta matokeo makubwa zaidi na yenye faraja,” amesema Mkinga aliyeongozana na viongozi wa juu wa umoja huo.

“Nawasisitiza wadogo zetu ambao wako katika field (mafunzo kwa vitendo) mbalimbali waendelee kuisikiliza Serikali juu ya mtalaa mpya ambao tunazungumza – mtalaa unaozingatia umahiri,” amesema.

Amesema katika kikao hicho wamepata majibu sahihi kwamba, kutokana na sheria na sera, yapo mambo ambayo hayawezi kubadilishwa kwa muda mfupi, ndiyo maana imeundwa timu hiyo kwa ajili ya maridhiano na kutatua changamoto walizoziwasilisha.

“Niwatangazie Watanzania kuwa haya si siasa. Wawe wastahimilivu, waendelee kudumisha umoja na kulinda amani yetu, kwani Mheshimiwa Rais (Rais Samia Suluhu Hassan), kupitia wawakilishi wake, wametupokea na kutusikiliza kama watoto wao,” amesema.

Amemshukuru Waziri Simbachawene kwa jinsi alivyowapokea, kuwasikiliza, na kujadiliana kuhusu changamoto zao.

Awali, Mwenyekiti wa Neto, Joseph Kaheza, amesema kwa kuzingatia falsafa ya 4R (maridhiano, mabadiliko, ustahimilivu, na kujenga upya) ya Rais Samia, walikutana na mazungumzo yao yalikuwa na tija.

“Nafasi hiyo imekuwa ya kipekee kwa kujadiliana na Serikali juu ya namna bora zaidi ambayo itasaidia na kuleta maendeleo kwa vijana wa Kitanzania na Taifa,” amesema.

Kikao hicho ni matokeo ya kauli ya Machi 3, 2025, ya Simbachawene aliyoitoa wakati akizungumza na wakuu wa taasisi na mashirika jijini Dodoma kuwa amepanga kukutana na vijana hao ili kuwasikiliza.

Alisema atakutana na vijana hao Machi 10, 2025, yeye pamoja na Profesa Mkenda na Mchengerwa, ili kuwasikiliza.

Harakati za umoja huo zinaungwa mkono na Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) Mkoa wa Mwanza, huku ukiitaka Serikali ichukue hatua za kupunguza changamoto ya ajira kwa vijana.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *