
Dodoma. Bunge limeidhinisha Sh277.04 bilioni kwa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kwa miradi ya maendeleo, ndani yake zikiwamo Sh73 bilioni zitakazotumika katika ujenzi wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano, ambao ni nguzo muhimu katika kukuza na kuboresha teknolojia ya habari na mawasiliano nchini.
Jumla ya fedha za Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari zilizoidhinishwa na Bunge leo Ijumaa Mei 16, 2025 ni Sh291.53 bilioni, ambapo Sh277.04 bilioni kati ya hizo zimewekwa kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo.
Akiwasilisha bajeti hiyo, Waziri mwenye dhamana na wizara hiyo Jerry Silaa, amesema kuwa wizara kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo na sekta binafsi, imepanga kutekeleza miradi saba mikuu kwa mwaka wa fedha 2025/26.
Silaa amesema miradi hiyo inalenga kuboresha upatikanaji wa huduma za mawasiliano zenye uhakika na gharama nafuu kwa wananchi.
Silaa amebainisha kuwa Sh73 bilioni zimetengwa kwa ajili ya utekelezaji wa ujenzi wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano, ambao ni msingi wa kukuza teknolojia ya habari na mawasiliano nchini.
“Katika mwaka 2025/26 wizara imekadiria kutumia Sh26.8 bilioni kwa ajili ya kuendelea na utekelezaji wa mfumo wa anwani za makazi,”amesema.
Amesema katika mwaka 2025/26 wizara inakadiria kutumia Sh2.1 bilioni fedha za ndani kwa ajili ya kutekeleza mradi wa kuendeleza ubunifu na utengenezaji wa vifaa vya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama).
Silaa amesema Sh12.8 bilioni zimetengwa kujenga vituo vya ubunifu wa Tehama, lengo likiwa ni kukuza ujuzi na ajira kwa vijana.
Aidha, Sh28.1 bilioni zitatumika kwenye mradi wa Tanzania ya Kidijitali na Sh3.0 bilioni kuimarisha taasisi za sekta hiyo.
Uhalifu mtandaoni
Kuhusu uhalifu wa mitandaoni, Waziri Silaa amesema jumla ya laini za simu 47,728 zimezuiwa kutumika, huku nambari za vitambulisho vya Taifa 39,028 zikiwa zimeorodheshwa (blacklisted) kutokana na kuhusishwa na matumizi yasiyofuata sheria.
Aidha, Silaa amesema TCRA kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama ilifanya operesheni ya ukaguzi na kufanikisha kukamatwa kwa vifaa 42 vilivyokuwa vikitumika kufanya uhalifu wa uchepushaji wa simu za kimataifa.
“Zoezi hili ni endelevu na linalenga kuziba mianya ya upotevu wa mapato pamoja na kuwalinda watumiaji wa huduma za mawasiliano nchini.
Aidha, Silaa amesema kuwa jumla ya namba tambulishi 44,306 zilifungiwa baada ya kuripotiwa kuwa zimepotea, kuibiwa au kuhusika na matukio ya kihalifu, hatua ambayo imesaidia kupunguza visa vya wizi na kuimarisha upatikanaji wa vifaa vya mawasiliano vyenye ubora kwenye soko.
Akiwasilisha maoni ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kuhusu makadirio hayo, Mjumbe wa kamati hiyo, Miraji Mtaturu amesema tatizo la uhalifu na utapeli kwenye mitandao ya mawasiliano bado linaendelea kwa kasi.
“Kamati inaendelea kuishauri Serikali kuwa, pamoja na hatua zinazoendelea kuchukuliwa na mamlaka husika, jitihada zaidi zinahitajika ili kutoa ufumbuzi wa kudumu sambamba na kuzuia jumbe fupi zinazotumwa bila idhini au matakwa ya mteja,”amesema.
Aidha, Mtaturu amesema wizara husika ishirikiane na makampuni ya mitandao ya simu pamoja na Wizara ya mambo ya ndani ili kumaliza tatizo hilo.