Naibu Waziri wa Fedha Mhe. Hamad Chande, akiwa na Mkurugenzi Mtendaji wa WFT-T Bi. Rose Marandu,(kulia), Profesa Penina Mlama (Kati) na Pembeni kushoto ni Mwakilishi Mkaazi wa Shrika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia wanawake (Unwomen) Hodan Haddou.
Na Deogratius Koyanga
Wizara ambazo hazitatenga Bajeti yenye mtazamo wa Kijinsia, zitatakiwa kutopewa fedha hadi zitakapozingatia mahitaji ya msingi ya makundi yote wakiwepo wanawake, wanaume, wazee watoto, wasichana na watu wenye ulemavu.
Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Mfuko wa ruzuku kwa wanawake (WFT-T) Profesa Penina Mlama mbele ya Naibu Waziri wa Fedha, Hamad Chande, Wakati wa maadhimisho ya sherehe za Miaka 30 ya Beijing, na siku ya wanawake Duniani, zilizoandaliwa na Mtandao wa wanawake, Katiba, Uongozi na uchaguzi chini ya uratibu wa WFT-T.
“Mhe. Naibu Waziri, tunaishukuru serikali, wakati tumeenda Beijing miaka 30 iliyopita, tuliaambatana na viongozi wa serikali, watumishi wa wizara mbalimbali na wawakilishi wa sekta. Hawa waliwezeshwa na wizara ya fedha. Masuala ya Beijing ambayo yametekelezwa hapa Tanzania, yametumia bajeti na fedha za serikali ambazo zinatoka katika wizara yako. Tunaona jinsi wizara ya fedha imewajibika kusimamia utekelezaji wa maamzimio ya Beijing” ,alisema Profesa Mlama na kuongeza:
“Tunakuomba kwa nafasi ya wizara hii, kwa kuzingatia kwamba bado tunahitaji bado fedha kutekeleza masuala haya 12 ya Beijing, wizara ambayo haitazingatia Bajeti yenye mtazamo wa Kijinsia, isipewe fedha”.
Mwongozo wa Taifa wa Bajeti kwa mwaka wa fedha 2025/2026, inazitaka wizara, Idara na mamlaka za Serikali za Mitaa kuzingatia bajeti yenye mrengo wa Kijinsia (GRB), katika Bajeti zao ambapo zitatakiwa kuzingatia Haki na mahitaji ya makundi maalum.
Kwa upande wake , Naibu Waziri wa Fedha Mhe. Hamad Chande amesema kwamba, serikali inazingatia na kuheshimu sana utekelezaji wa masuala yote 12 ya Beijing, na kuhakikisha kila sekta inatekeleza na kuweka rasilimali zitakazowezesha kuondoa mapungufu ya usawa wa Kijinsia nchini.
“Sisi zote tumetunzwa na kulelewa na kina mama, tunahitaji kuwahshimu kwa kuweka miundombinu safi na salama katika kuboresha maisha yao, hili ni deni kwetu sote, tunatakiwa kuwajibika kufanya hivyo”, alisema.
Akizungumza, aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, na Kiongozi wa Mkutano wa Beijing, Balozi Getrude Mongela, alisema kwamba serikali inatakiwa kufuatilia namna ambavyo wanawake wananufaika na bajeti inayotengwa na serikali ili kuondoa tatizo la mnyororo wa thamani kwa wanawake wakulima wa Tanzania.
“Nakuomba ukafuatilie, fedha za bajeti zinazotengwa zinaishia wapi?, zinawafikia wanawake? Fedha hizi za bajeti zinazokusanywa na serikali zinatoka mifukoni mwa wanawake, hii miradi mikubwa ya maendeleo inawanufaisha wanawake?”, alisema Balozi Mongela na kuongeza:
“Nenda hatua kwa hatua ukokotoe bajeti ya kilimo, ambayo wanawake wengi wamewekeza nguvu zao huko, fedha kiasi gani zinakwenda kuwezesha wanawake kujenga viwanda vya kuongeza dhamani ya mazao yao? Angalia ni fedha kiasi gani zimeenda kwenye vikundi vya wanawake?”.
“Miaka 80 yangu, natamani kuona jembe la mkono limeondoka, kutumia teknolojia katika kilimo ili kumuondolea mwanamke mzigo wa kazi, natamani kuona naibu waziri kusimamia bajeti ya kilimo, ikiondoa mzigo kwa wanawake”,aliongeza Balozi Mongela.
Kongamano hili la Kitaifa, lenye kauli mbiu ya Kusherehekea Miaka 30+ Beijing: Tumetoka wapi, Tulipo, na Tuendako, pamoja na mengine malengo yake ni pamoja na Kutoa nafasi kwa wanaharakati wa harakati za wanawake nchini kusherehekea hatua muhimu na kuheshimu historia ya harakati za ukombozi wa wanawake;
Pia kufikiria upya maisha ya wanawake baada ya Beijing +30, kuchambua hali ya sasa, changamoto na jinsi changamoto za wanawake zinavyokabiliwa pamoja na matokeo yake;
Aidha lengo jingine ni kujenga mitandao, kujifunza, kuunda pamoja taasisi za kimabadiliko, na kuunganisha nguvu kwa mustakabali wa pamoja.
The post WIZARA ISIPOTENGA BAJETI YENYE MTAZAMO WA KIJINSIA INYIMWE FEDHA – PROF. MLAMA appeared first on Mzalendo.