‘Wivu’ wa Jay Combat ulivyompa shavu Mushizo

Dar es Salaam, Muziki wa Singeli kwasasa ni miongoni mwa aina za muziki pendwa nchini Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla, hiyo ni kutokana na utofauti wake katika mapigo na midundo ambayo huwa imechangamka na kuwa ya haraka zaidi.

Muziki huo ambao asili yake ni uswahilini umeendelea kukua na kusambaa kwenye mataifa mengine kutokana na ukuaji wa mitandao ya kijamii na hiyo hupelekea kujizolea mashabiki wapya kila kukicha.

Lakini kama wasemavyo Waswahili safari moja huanzisha nyingine wakiwa na maana ya jambo moja linaweza kuwa mwanzo wa jambo lingine ndivyo ilivyokuwa kwa wimbo unaotamba ‘Wivu’ ambao awali ulifanywa na mwanamuziki wa Singeli Jay Combat na kisha baadaye kufanyiwa remix na Dj Mushizo ambaye kwa sasa ndiye mmiliki wa remix hiyo.

Dj Mushizo ambaye kwa sasa anatamba zaidi kama Dj wa matamasha ya muziki wa Singeli, mwimbaji na  mzalishaji wa muziki huo akiwa amemshirikisha Jay Combat, Ibraah, na Baddest 47 kwenye ‘Wivu’ remix aliiambia Mwananchi kabla ya kufanya remix alikutana na kionjo cha wimbo huo kwenye mitandao ya kijamii.

“Mara ya kwanza huu wimbo niliusikia kupitia TikTok ilikuwa ni shoo ya Jay Combat nikamcheki akaniambia wimbo umeshatoka lakini haukufanya vizuri nikamwambia huu wimbo nataka tuufanye kwa ukubwa maana tayari mimi nimejuana na wasanii wakubwa nafahamu promosheni ya muziki.

“Nilikuwa na uwezo wa kufanya huu wimbo mimi kama Mushizo na Jay Combat lakini nikasema hapana nikakaa na uongozi wangu tukashirikiana tukaona mtu anayefaa ni Baddest 47 nikamcheki akafanikisha jambo, Mungu akabariki Ibraah akapenda na yeye akabiriki vesi moja na mpaka sasa ndio ngoma namba moja na sasa hivi mimi ndio mmiliki wa wimbo huo,” amesema Mushizo.

Hata hivyo, kutokana na wengi kumfahamu Mushizo kama Dj wa muziki anasema alianza kujitafuta kama dansa na mwimbaji kisha suala la U-dj ambalo limempatia umaarufu likafuata.

“Nilikuwa napenda kazi ya kupiga muziki nikawa napenda sana Dj akiwa anafanya vile, nikawa najifunza  nakumbuka kazi yangu ya kwanza ilikuwa Kivule, unajua wasanii na Ma-dj wengi wa singeli wanapewa sapoti na masala,  watu wa mtaani sasa mwaka 2014 nikiwa kwenye kigodoro kuna Dj alikuwa anapiga mabraza kama 6 wakamkoromea wakamtoa wakaniweka pale ilikuwa noma sana watu walinipokea kwa ukubwa,” amesema Mushizo.

Mushizo anasema safari yake kwenye muziki wa singeli iliendelea kukua hadi kufikia hatua ya kupokea simu za biashara kutoka kwa watu mbalimbali.

“Tulihama tukahamia Msongola Mbagala huko nikawa napiga mabiti yangu muda huo bado sijapata msanii yoyote wa kuniamini ila mabiti yangu yakawa yanapigwa tu na bodaboda na bajaji, nakumbuka ilikuwa mwaka 2018 ndio nilipokea simu yangu ya kwanza ya kazi kutokea Rufiji walionipigia wakaniambia tunaomba uje kufanya shoo huku.

“Kiukweli nilikuwa naogopa nikawakaushia kama siku 4 sijawajibu wakanitafuta tena ikabidi niombe ushauri kwa washikaji na ndugu zangu tukawapigia na tukaelewana vizuri ila pesa yao haikuwa kubwa haikufika hata laki moja lakini ndio ilikuwa shoo yangu ya kwanza nilipokelewa kama mfalme mpaka wanangu (rafiki) nilioongozana nao wakawa wanashangaa,”amesema Mushizo. 

Mushizo aliendelea kuiambia Mwananchi kuwa ndoto yake tangu zamani ni kukua kila siku japo shoo yake ya kwanza haikumpatia pesa za kutosha kuna kitu ilimjengea kwenye mapambano yake na ndio ilimsaidia hadi kukutana na msanii wa singeli wa kwa kwanza ambaye aliamini uwezo wake na kumpa nafasi ya kufanya naye kazi.

“Mwaka 2020 nilipata bahati nikakutana na Balaa Mc, Mungu akabariki tukafanya wimbo wa ‘Nakuja’ hapo nikaanza kutambulika kwa ukubwa shoo zikawa nyingi na nikaanza kufahamikana na watu maarufu mambo yakafunguka,”amesema Mushizo.

Utofauti muhimu kwa msanii 

Moja ya kitu kinachomfanya msanii kutambulika zaidi na kuendelea kufanya vizuri ni ubunifu, upekee na utofauti wa kazi zake Mushizo licha ya kuanza kupata mafanikio kwenye muziki wa singeli kupitia kazi alizofanya na wasanii wa muziki huo haikumfanya aache kupiga biti za singeli na kuchanganya aina nyingine ya muziki.

“Singeli ninayofanya mimi ya kitofauti ndio maana mashabiki wananikubali kwa sababu kuna vitu ambavyo huwezi vipata kwa Dj mwingine zaidi yangu, kwa mfano kama sasa hivi nangoma zangu ambazo nimewashirikisha wasanii kama ‘Nimemposti’, ‘Wivu’ ni nyimbo ambazo zime-hit, mimi nafanya kazi na wasanii wote mfano nafanya na Balaa Mc, Meja Kunta,” amesema.

Mushizo kuhamia kwenye Bongo Fleva

Imezoeleka kuona wasanii wa Bongo Fleva wakifanya muziki wa singeli na aina nyingine ya muziki aidha kwa baadhi ya  wasanii wa singeli pia wamekuwa wakifanya aina tofauti na muziki wao mfano Dvoice msanii kutokea lebo ya muziki nchini WCB, na hata Balaa Mc amekuwa akinata na biti za hip-hop, lakini hiyo imekuwa tofauti kwa Mushizo.

“Ni vizuri wao wakifanya muziki tofauti lakini kwa sasa natamani watu wanielewe kupitia muziki huu wa singeli sitaki nichanganye vitu, sio kwamba siwezi kufanya muziki wa aina nyingine ila nataka watu wanijue zaidi kupitia singeli maana sasa hivi ukisema ‘WEEE MUSHIZOO’ watu wanajua nini kinafuata,”amesema Mushizo.

Muziki wa Singeli ni uhuni?

“Kwa sasa wanamuziki wa singeli sio wahuni kabisa kama watu wanavyofikiria wasanii wengi wanajielewa ukiniangalia mimi nipo smati na wasanii wenzangu wengi tupo vizuri tunamiliki biashara zetu tunatunza familia kiukweli tunaishi vizuri kwa hiyo dhana ya uhuni ilikuwa zamani kama unavyojua kila jambo likianza changamoto hazikosi kwa hiyo ni kazi tu kama zingine,”amesema.