Wingi wa nta kwenye sikio: janga jipya la kutosikia

Moshi. Watu 413 kati ya 1,598 waliofanyiwa uchunguzi wa usikivu katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini, KCMC, wamebainika kuwa na tatizo la kutokusikia, huku chanzo kikubwa kikitajwa kuwa ni wingi wa nta kwenye masikio.

Akizungumzia changamoto hiyo leo, Machi 4, 2025, Mkuu wa Idara ya masikio, pua na koo  katika Hospitali ya KCMC, Dk  Desderius Chussi, amesema kuwa asilimia 45 ya watu waliofanyiwa uchunguzi walibainika kuwa na matatizo ya kutosikia kutokana na kuzalishwa kwa nta nyingi kwenye sikio.

Amesema uwepo wa nta nyingi kwenye sikio kunasababisha kuziba, hivyo upitishaji wa sauti hadi kwenye ngoma ya sikio unakuwa na hitilafu.

“Kati ya wananchi 1,598 tuliowafanyia uchunguzi wa masikio na usikivu, 413 walikuwa na nta iliyokithiri, ambayo ni sawa na asilimia 45 ya waliofanyiwa uchunguzi. Walisafishwa, na wengine walipatiwa dawa za kulainisha na kusafisha nta,” amesema Dk Chussi.

Dk Chussi amesema  kuwa, vipimo vya audiolojia (usikivu) vilivyofanyika kwa watu 117, ambao ni asilimia 25 ya waliogundulika kuwa na matatizo ya usikivu, walipatiwa vifaa maalumu vya usikivu.

Mkurugenzi Mtendaji wa KCMC, Profesa Gileard Masenga amesema  hospitali hiyo inaendelea kutoa huduma za uchunguzi katika idara ya masikio na wanaobainika kuwa na matatizo wanapatiwa matibabu sahihi.

“Idara yetu ya masikio, pua na koo ni bingwa na bobezi hapa KCMC,  hivyo tunaendelea kutoa huduma za uchunguzi wa masikio na usikivu, na tumetembelea shule mbalimbali ambapo tumebaini matatizo ya usikivu kwa baadhi ya wanafunzi na kuwapatia tiba.”amesema Profesa Masenga

Baadhi ya watumishi wa idara ya Masikio Pua na Koo(NIT) wa hospital ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini, KCMC wakiwa katika viwanja vya hospitali hiyo.Picha na Janeth Joseph

Mmoja wa madaktari kutoka kitengo hicho, Michael Kayuza ameeleza kuwa  changamoto ya nta nyingi kwenye sikio ni kubwa na wapo baadhi ya watu ambao huzalishwa kwa wingi kwenye masikio yao.

“Nta nyingi kwenye sikio ni tatizo kubwa linaloonekana hasa kwa wazee na watu wazima, na hii inasababisha sikio kuziba kwa hiyo upitishaji wa sauti hadi kwenye ngoma ya sikio unakuwa na hitilafu, hivyo mtu anakosa kusikia vizuri.”amesema Dk Kayuza