
Buchosa. Wavuvi wanaovua samaki aina ya dagaa ndani ya Ziwa Victoria wameiomba Serikali kuwaondolea wingi wa kodi unaoathiri shughuli zao za uvuvi ndani ya ziwa hilo.
Kauli hiyo imetolewa na mwenyekiti wa wavuvi wa dagaa, Juma Bupamba kwenye mwalo wa Gembale (Kisiwani) uliopo Kata ya Bulyaheke kuwa wingi wa kodi umekuwa mwiba kwenye shughuli zao za uvuvi.
Amesema mwanzoni mwa mwezi huu wafanyakazi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), walikwenda kisiwani hapo na kutoa elimu inayomtaka kila mvuvi mwenye zana za uvuvi kulipia kodi.
Kwa mujibu wa Bupamba kodi ya kila mtumbwi ni Sh250,000 kwa mwaka fedha zitakazokwenda Serikali kuu.
Hata hivyo, Kaimu Meneja wa TRA Mkoa wa Mwanza, Julius Mafuru, amesema kuwa kila Mtanzania anapaswa kulipa kodi na kwamba jambo hilo lipo kisheria.
Amesisitiza kwamba kila mmiliki anapaswa kulipa kodi hiyo, na wataendelea kutoa elimu ili jamii ielewe umuhimu wa ulipaji kodi kwa maendeleo ya Taifa.
Hata hivyo, Bupamba amesema mbali na kodi hiyo ya TRA, wanalipa leseni ya mtumbwi Sh120,000 kila mwaka inayolipwa kwenye Halmashauri ya Buchosa, wanalipa Sh84,000 fedha zinazokwenda Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (Tasac), hivyo ongezeko ya la Sh250,000 za TRA zinawaongezea wingi wa kodi kiasi cha kuwafanya washindwe kumudu shughuli zao za uvuvi.
” Kama Serikali haitasikia kilio chetu tuko tayari kufunga uvuvi hadi tutakaposikilizwa,” amesema Bupamba.
Katibu Msaidizi wa chama cha wavuvi wa dagaa Kanda ya Ziwa Victoria, Hassan Muhenga amesema Serikali inatakiwa kuwaonea huruma wavuvi kama inavyowaonea huruma wakulima.
Huku akidai kodi ya TRA imekuja kuwafilisi wavuvi, amesema hakuna mvuvi anayeweza kumudu kulipa kodi hiyo ambayo haikuwepo zamani.
” Sisi hatupingani na Serikali tunachoomba ni kuweka usawa siyo kuumiza wavuvi, amesema Muhenga.
Kwa upande wake mvuvi Gidwin Sebastiani wa mwalo wa Gembale naye anapinga ongezeko la kodi hiyo ya TRA kwa kuwa imewaongezea mzigo kiasi cha kufikiria wafunge uvuvi.