
Shirika la Afya Duniani (WHO) limetangaza kuwa, zaidi ya watu 50,000 kufikia sasa wamechanjwa dhidi ya virusi vya mpox katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Rwanda.
Maafisa wa WHO wanasema kuwa, zoezi la utoaji chanjo linaendelea vizuri ikiwa ni katika juhudi za kukabiliana na maradhi hayo hatari.
Wakati huo huo shirika la afya la Umoja wa Afrika limeonya na kutoa wito wa kupatikana kwa rasilimali zaidi ili kuepuka janga hilo kuwa kubwa kuliko janga la Uviko 19 la miaka michache iliyopita.
Kwa mujibu wa ripoti ya Vituo vya Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa Afrika (CDC), zaidi ya watu 1,100 wamekufa kwa ugonjwa wa mpox barani Afrika, na takriban watu 48,000 wameorodhoshwa kuwa wameambukizwa tangu Januari mwaka huu.
Mpox ni ugonjwa unaosababishwa na virusi, ambao hapo awali ulijulikana kwa jina la ugonjwa wa tumbili, kabla ya Shirika la Afya Duniani (WHO) kubadili jina lake mwaka wa 2022 kutokana na malalamiko kwamba jina hilo linaibua hisia za ubaguzi na unyanyapaa.
Ugonjwa huo unaweza kuambukizwa kwa wanadamu kwa kuwasiliana kwa karibu na mtu aliyeambukizwa au na mnyama mdogo wa mwituni, au kupitia vifaa vyenye maambukizi.