
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) amesema, kupiga marufuku shughuli za Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA) hakufanyi utawala wa Kizayuni kuwa salama zaidi.
Bunge la Kizayuni (Knesset) Jumatatu ya tarehe 28 Oktoba, lilipitisha mswada wa kupiga marufuku shughuli za shirika hilo la msaada kwa Wapalestina.
Muswada mwingine pia umepitishwa ambao unapiga marufuku na utawala huo pandikizi kushirikiana na UNRWA.
UNRWA ni Shirika la Umoja wa Mataifa la Msaada na Kazi kwa Wakimbizi wa Kipalestina ambalo ni mojawapo ya mashirika makubwa ya kutoa misaada katika Ukanda wa Gaza, likiwa na wafanyakazi wapatao 13,000 ambao wamekuwa wakifanya kazi wakati wote wa vita huko Gaza.
Mbali na usambazaji wa chakula, UNRWA hutoa elimu na huduma za kimsingi za matibabu katika ukanda huo, na kwa sasa wafanyakazi elfu tatu wa wakala huo wanaendelea kufanya kazi za kutoa huduma za dharura kwa Wapalestina madhulumu huko Gaza.
Kwa mujibu wa ripoti ya kanali ya Sahab leo Jumanne,”Tedros Adhanom Ghebreyesus”, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), alisema jana kwamba hakuna mbadala wa UNRWA, na kuongeza kama ninavyomnukuu: ‘Kupigwa marufuku UNRWA kutaongeza tu mateso kwa watu wa Ukanda wa Gaza na kuongeza hatari ya kuzuka magonjwa.’
Huku Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa likionya dhidi ya jaribio lolote la utawala katili wa Kizayuni la kukwamisha shughuli za UNRWA, Kituo cha Televisheni cha utawala huo cha Kanali ya 12 kiliripoti jana Jumatatu kwamba Tel Aviv imeufahamisha rasmi Umoja wa Mataifa kwamba imekata uhusiano na shirika hilo.