
Dar es Salaam. Shirika la Afya Duniani (WHO) linapanga kupunguza idadi ya wafanyakazi na kiwango cha kazi, huku likipunguza bajeti yake kwa zaidi ya asilimia 20 kutokana na athari za kupunguzwa kwa ufadhili wa Marekani.
Uamuzi huo umo kwenye taarifa ya ndani zilizoripotiwa na Shirika la Habari la Uingereza (Reuters), ikitolewa na Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Dk Tedros Adhanom Ghebreyesus kwa wafanyakazi.
Januari 20, Serikali ya Rais wa Marekani, Donald Trump ilijiondoa kutoka WHO, uamuzi uliokuwa moja ya maagizo ya kwanza ya kiongozi huyo baada ya kuapishwa, akidai shirika hilo lilishughulikia vibaya janga la Uviko19 na migogoro mingine ya afya ya kimataifa.
Marekani ndiye alikuwa mfadhili mkuu wa kifedha wa WHO, ikichangia takriban asilimia 18 ya ufadhili wake wote.
“Tangazo la Marekani, pamoja na kupunguza kwa misaada rasmi ya maendeleo katika baadhi ya nchi ili kufadhili ongezeko la matumizi ya ulinzi, limefanya hali yetu kuwa mbaya zaidi,” ilisema taarifa ya WHO iliyotolewa Machi 28, 2025 na kutiwa saini na, Dk Tedros.
Kuondoka kwa Marekani kumezidisha mgogoro wa kifedha kutokana na nchi wanachama kupunguza matumizi yao ya maendeleo.
Kukabiliana na pengo la mapato la karibu dola milioni 600 mwaka huu, WHO imependekeza kupunguza bajeti yake kwa mwaka 2026/2027 kwa asilimia 21 kutoka dola 5.3 bilioni hadi dola 4.2 bilioni, imesema taarifa hiyo.
Februari mwaka huu, Bodi ya WHO ilikuwa tayari imepunguza bajeti iliyopendekezwa kwa mwaka 2026/2027 kutoka dola 5.3 bilioni hadi dola bilioni 4.9.
“Licha ya jitihada zetu zote, sasa tumefikia hatua ambayo hatuna budi ila kupunguza kiwango cha kazi yetu na wafanyakazi,” ilieleza taarifa hiyo.
WHO itapunguza nafasi za kazi katika uongozi wa juu katika makao yake makuu huko Geneva, Uswisi, ingawa viwango vyote na kanda zote zitaathirika, taarifa hiyo iliongeza.
Yatafanyika maamuzi kuhusu jinsi ya kuzingatia vipaumbele vya kazi yake na rasilimali zake ifikapo mwishoni mwa Aprili.
Nyaraka za WHO zinaonyesha kuwa shirika hilo la Umoja wa Mataifa lina zaidi ya robo ya wafanyakazi wake 9,473 huko Geneva.
Taarifa ya ndani ya Machi 10, ambayo pia imenukuliwa na Reuters, imesema Shirika la Afya Duniani lilikuwa limeanza kuweka vipaumbele na kutangaza ukomo wa mwaka mmoja kwa mikataba ya wafanyakazi.
Taarifa hiyo imesema kuwa wafanyakazi walikuwa wakifanya kazi, kuhakikisha ufadhili wa ziada kutoka kwa nchi, wafadhili binafsi na mashirika ya hisani unapatikana.
Wadau mbalimbali wa masuala ya afya nchini, wamesema Marekani kujiondoa WHO ni pigo kubwa kwa mataifa masikini na nchi zinazoendelea, ikiwemo Tanzania.
Mwenyekiti wa Chama cha watoa huduma za afya binafsi Tanzania (Aphfta), Dk Egina Makwabe amesema Marekani inachangia asilimia 30 ya bajeti ya WHO, “Ukiangalia upande wa chanjo pale Gavi ule mpango wa kutoa chanjo kwa nchi masikini Marekani ndiyo ilikuwa mchangiaji mkubwa.”
Awali Trump alisema uamuzi wa Marekani kujitoa WHO ulitokana na hisia kwamba nchi yake ilikuwa na mzigo mkubwa zaidi kifedha ukilinganisha na China.
Marekani, yenye watu takribani milioni 331, ilichangia Dola 500 milioni za Marekani (Sh1.242 trilioni) kwa mwaka, huku China, yenye watu bilioni 1.4, ikichangia Dola 39 milioni (Sh96.110 bilioni) pekee.
Hata hivyo, wakati wa urais wake wa awali (2017–2021), mpango wake wa kuiondoa Marekani kutoka WHO ulizimwa na Rais Joe Biden baada ya kushinda uchaguzi wa 2020.
Zaidi ya robo ya fedha za Marekani Dola 158 milioni (Sh392.601 bilioni) zilitengwa kwa kampeni za kutokomeza polio duniani.
Miradi mingine mikubwa ni pamoja na afya bora na lishe Dola 100 milioni (Sh248.489 bilioni), utoaji wa chanjo dhidi ya magonjwa yanayozuilika Dola 44 milioni (Sh109.335 bilioni) na mapambano dhidi ya kifua kikuu Dola 33 milioni (Sh81.999 bilioni).
Fedha nyingine zilitengwa kwa miradi ya kupambana na Ukimwi, homa ya ini, magonjwa ya kitropiki, afya ya uzazi, upatikanaji wa dawa na hatua za kudhibiti majanga.