
Shirika la Afya Duniani (WHO) linasema kuwa litaendelea kuwa macho dhidi ya ugonjwa hatari wa mpox katika kiwango cha juu zaidi huku kukiwa na ongezeko la wagonjwa.
Kamati ya WHO inayoundwa na wataalamu huru zaidi ya 10 ilifanya uamuzi huo katika mkutano huko Geneva mnamo Ijumaa, miezi mitatu baada ya kutangaza dharura ya afya ya umma duniani mwezi Agosti.
WHO imesema uamuzi wake “unatokana na kuongezeka kwa idadi ya waliombukizwa na kuenea kijiografia, changamoto za matibabu, na hitaji la kuongeza na kudumisha mwitikio wa mshikamano katika nchi husika na washirika”.
Kumekuwa na ongezeko la visa vya mpox mwaka huu, ambavyo vimeshuhudiwa zaidi katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na nchi jirani.
Kundi la kwanza la chanjo lilitolewa mwezi uliopita na inaonekana kuwa na athari katika kudhibiti kesi za ugonjwa huo.
Shirika la Umoja wa Afrika la Kudhibiti Magonjwa linalosimamia masuala ya afya lilionya mwishoni mwa Oktoba kwamba mlipuko wa mpox bado haujadhibitiwa na kutaka rasilimali zaidi kuepusha janga ambalo linaweza kuwa mbaya zaidi kuliko COVID-19.
Mpox inaaminika kuua mamia ya watu nchini DRC na kwingineko mwaka jana huku ikisambaa hadi Burundi, Kenya, Rwanda, Nigeria na Uganda.