Wenye Uviko-19 waongezeka, Dar yatajwa

Wenye Uviko-19 waongezeka, Dar yatajwa

Dar es Salaam. Takwimu zilizotolewa na Wizara ya Afya zinaonyesha kuwepo ongezeko la watu wenye maambukizi ya ugonjwa wa Uviko-19 nchini katika kipindi cha miezi mitatu iliyopita.

Takwimu hizo zimetolewa leo Jumanne Mei 20, 2025, na Ofisi ya Mganga Mkuu wa Serikali, Dk Grace Magembe kupitia taarifa yake kwa umma, ambapo amesema kumekuwepo ongezeko la tetesi zinazohusiana na magonjwa ya mfumo wa njia ya hewa katika jamii nchini.

“Hali ya kuongezeka na kupungua kwa ugonjwa huu imekuwepo kila mwaka tangu kutangazwa kwa ugonjwa huu mwaka 2020. Kwa kipindi hiki ongezeko hili linaonekana zaidi katika Mkoa wa Dar es Salaam,” amesema Dk Magembe.

Dk Magembe amesema kupitia mfumo wa ufuatiliaji wa magonjwa ya mfumo njia ya hewa, wizara imebaini kuna ongezeko la wagonjwa wenye Uviko-19 kutoka wawili kati ya watu 139 waliopimwa Februari sawa na asilimia 1.4 hadi wagonjwa 31 kati ya watu 185 waliopimwa Aprili mwaka huu, sawa na asilimia 16.8.

“Tangu Februari hadi Aprili 2025, ufuatiliaji wa virusi hivi umeonesha ongezeko la visa vya UVIKO-19 kutoka asilimia 1.4 (wagonjwa wawili kati ya watu 139 waliopimwa) Februari hadi asilimia 16.3 (wagonjwa 31 kati ya 190 waliopimwa) Machi,” amesema Dk Magembe.

Aidha, Dk Magembe amewataka wananchi kuzingatia kanuni za afya kujikinga na kuwakinga wengine dhidi ya maambukizi ya magonjwa ya mfumo wa njia ya hewa.

“Njia za kujikinga ni pamoja na kufunika pua na mdomo wakati wa kukohoa au kupiga chafya, pamoja na kuvaa barakoa pale inapohitajika, kunawa mikono kwa maji tiririka na sabuni au kutumia vipukusi mara kwa mara na kudumisha usafi wa mwili binafsi na wa mazingira yanayotuzunguka,” amesema.

Dk Magembe amewataka wananchi kufuata hatua za kitaalamu wanapohisi changamoto ya kiafya kwa kile anachodai dalili zake ni vigumu kubainika bila uchunguzi wa wataalamu na vipimo vya maabara.

“Hivyo, nawasihi kuwahi katika vituo vya kutolea huduma mara mnapopata dalili zozote za homa, maumivu ya kichwa, macho, misuli, viungo, au vipele mwilini au dalili za magonjwa ya mfumo wa njia ya hewa kama vile kikohozi, mafua, kuwashwa koo au kupumua kwa shida ili kupata vipimo na matibabu stahiki,” amesema.

Katika hatua nyingine, Dk Magembe amesema vipimo vya maabara vimebaini kuongezeka na kupungua kwa virusi vya Influenza (Seasonal Influenza) nchini (bila kutaja idadi).

“Aidha vipimo hivyo vimeonesha kuwa hakuna kirusi kipya kinachoweza kusambaa kwa haraka na kusababisha mlipuko wa aina ya pandemiki. Tutaendelea kutoa taarifa sahihi kwa wakati kwa lengo la kuwalinda na kuhakikisha usalama wa afya za Watanzania wote,” amesema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *