
Dar es Salaam. Mkurugenzi wa kampuni ya mikopo ya Atlantic Micro Credit Limited, Wendy Ishengoma (38) na wenzake watatu ambao wanakabiliwa na kesi ya kuendesha biashara ya upatu, wataendelea kusota rumande hadi Machi 12, 2025 kesi hiyo itakapotajwa.
Hatua hiyo inatokana na upelelezi wa kesi hiyo kutokamilika, huku mashitaka yanayowakabili hayana dhamana kwa mujibu wa sheria.
Wendy na wenzake watatu wanakabiliwa na mashitaka ya kuongoza genge la uhalifu, kuendesha biashara ya upatu na kutakatisha Sh3.6 bilioni, katika kesi ya uhujumu uchumi.
Leo Jumatano Machi 5, 2025, Wakili wa Serikali, Cathbert Mbilingi ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kuwa uchunguzi wa shauri hilo bado unaendelea.
Mbilingi ametoa taarifa hiyo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Aaron Lyamuya, wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya kutajwa.
Wendy, ambaye alijifungua mtoto wa kiume Februari 21, 2025 akiwa gerezani, ameshindwa kufika mahakamani hapo kwa mara ya pili, kusikiliza kesi yake kutoka na kuwa kwenye uzazi.
Hata hivyo washtakiwa wenzake, wameiomba Mahakama hiyo, tarehe ijayo Ishengoma aletwe mahakamani hapo ili aungane na wenzake kusikiliza mwenendo wa kesi yake.
Pia washtakiwa hao wamedai kuwa kesi yao imefikisha siku 152 bila upelelezi kukamilika huku wao wakiwa rumande, hivyo wanaomba upande wa mashitaka wakamilishe kwa haraka uchunguzi. Hakimu Lyamuya baada ya kusikiliza maelezo ya pande zote mbili aliahirisha kesi hiyo hadi Machi 12, 2025 saa tano asubuhi.
Mbali na Wendy, washtakiwa wengine ni Sultan Mdee (29) Mhasibu na mkazi wa Goba; Frank Tengia (34) Meneja tawi na mkazi wa Mbezi Juu, pamoja na Mwiga Mwiga (31) ambaye ni Ofisa Masoko wa kampuni hiyo.
Itakumbukwa kuwa Januari 17, 2025 Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP), alimfutia Wendy shitaka la kutakatisha fedha.
Kutokana na kufutiwa shitaka hilo Wendy, sasa atakuwa na mashitaka mawili huku wenzake wakiwa na mashitaka matatu.
Licha ya kufutiwa shitaka la kutakatisha ambalo linampa nafasi Wendy kwenda kuomba dhamana Mahakama Kuu, mshtakiwa huyo ameshindwa kwenda kuomba dhamana na hivyo anaungana na washtakiwa wenzake kuendelea kusota rumande.
Alidai katika shitaka la kwanza ni kuongoza genge la uhalifu, linalowakabili washtakiwa wote wanne, ambapo wanadaiwa kati ya Januari 18, 2024 na Oktoba 11, 2024 ndani ya Jiji la Dar es Salaam, kwa makusudi washtakiwa wote waliongoza na kusimamia genge la uhalifu kwa kufanya biashara ya upatu.
Shitaka la pili ni kuendesha biashara ya upatu, linalowakabili washtakiwa wote, tukio wanalodaiwa kulitenda kati ya Januari 18, 2024 na Oktoba 11, 2024 ndani ya Jiji la Dar es Salaam.
Inadaiwa washtakiwa katika kipindi hicho, walifanikisha mpango wa kuendesha biashara ya upatu kwa kutoa ahadi kwa wanachama na kuingia mikataba ya ubia yenye thamani ya Sh 3,631,761,863, kitendo ambacho ni kinyume cha sheria.
Shitaka la tatu ni kutakatisha fedha, linalowakabili washtakiwa watatu ambao ni Mdee, Tengia na Mwiga.
Inadaiwa kuwa katika kipindi hicho ndani ya Jiji la Dar es Salaam, walijipatia Sh3,631,761,863 wakati wakijua kuwa wanapokea fedha hizo ni mazalia ya kosa tangulizi la jinai ambalo ni kuendesha biashara ya upatu.
Baada ya kusomewa mashitaka, upande wa mashitaka ulidai kuwa upelelezi haujakamilika hivyo wanaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa. Kwa mara ya kwanza, washtakiwa hao walifikishwa mahakamani hapo Oktoba 29, 2024 na kusomewa mashitaka hayo.