Wema Sepetu awasili Bodi ya Filamu kusikiliza kesi yake 

Wema Sepetu awasili Bodi ya Filamu kusikiliza kesi yake 

Dar es Salaam. Mwigizaji Wema Sepetu tayari amewasili Bodi ya Filamu baada ya kutakiwa kufika leo  Mei 22, 2025 saa 4 asubuhi kwa ajili ya mahojiano.

Wito huo ni ule uliosababishwa na picha jongefu zilizorushwa kwenye mtandao wa kijamii zikionyesha amevaa mavazi yanayodaiwa kutokuwa ya staha.

Kutokana na hayo Kaimu Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu Tanzania, Dk Gervas Kasiga Mei 19,2025 alimtaka msanii huyo kufika katika ofisi za bodi hiyo kwa ajili ya mahojiano.

Taarifa ya wito huo iliandikwa ” Mwanatasnia Wema Abraham Sepetu unatakiwa kufika ofisi za Bodi ya Filamu Tanzania. Bodi ya Filamu ni chombo kilichoundwa kisheria kutengeneza na kulinda taswira ya taifa letu pamoja na kuendeleza sekta ya Filamu nchini.

“Katika kutimiza majukumu hayo haiwezi kuacha kusimamia masuala ya nidhamu na maadili kwa wanatasnia wetu.Bodi imesikitishwa na picha jongevu zisizokuwa na maadili zilizorushwa kwenye mitandao ya kijamii zikimuonesha Mwanatasinia Wema Sepetu akiwa katika mavazi yasiyo na staha.

“Hivyo, Bodi inamtaka mwanatasinia husika (Wema) kufika bila kukosa katika Ofisi za Bodi ya Filamu zilizopo Kivukoni – Dar es Salaam Siku ya Alhamisi, Tarehe 22 Mei, 2025, Saa Nne Asubuhi kwa ajili ya mahojiano.”

Utakumbuka  wikiendi iliyopita Wema alionekana akiwa amevaa vazi ambalo linadaiwa kwamba halikuwa na staha  kwenye sherehe ya kujipongeza kupata tuzo ya thamani nchini Kenya.

Picha hiyo ilipokea maoni mbalimbali kwa watumiaji wa mitandao ikiwemo ya ukosoaji huku wengine wakilitetea vazi hilo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *