Wema na Diamond ni alama isiyofutika

Dar es Salaam. Ni miaka zaidi ya 10 imepita tangu Wema Sepetu na Diamond Platnumz wameachana lakini uhusiano wao una alama uliyoacha katika tasnia ya muziki Bongo licha ya drama nyingi walizopitia pamoja kwa kipindi chote cha penzi lao.

Wema, Miss Tanzania 2006 kwa asilimia kubwa alimfanya Diamond kuwa maarufu zaidi baada ya muziki wake, alimkaribisha katika ulimwengu wa kuangaziwa sana na vyombo vya habari na mitandao ya kijamii.

Inajulikana tayari Wema alikuwa maarufu kupitia Miss Tanzania pamoja na filamu alizocheza ikiwemo A Point of No Return (2007), Family Tears (2008), Red Valentine (2009), White Maria (2010) n.k.

Kulingana na Wema, mara ya kwanza kuonana ana kwa ana ilikuwa katika klabu ya usiku, Bilicanas ambapo Diamond alikuwa eneo maalamu la kuvutia sigara na rafiki zake, walitazamana tu kwa mbali na hakuna aliyemsalimia mwenzake.

Wakati huo Diamond alikuwa akifanya vizuri na nyimbo zake mbili, Kamwambie (2009) na Mbagala (2010), baada ya muda Wema aliyekuwa anatoka na Chazz Baba kipindi hicho, akaenda Marekani kwa dada yake.

Alipofika dada yake akamuuliza kama ana namba ya Diamond maana nyimbo zake zinafanya vizuri Marekani hivyo anaweza kwenda kufanya show huko, basi Wema akamuomba Ray C ampatie namba ya Diamond, na punde tu wakawasiliana na kumueleza hilo.

Basi wakaendelea kuwasiliana mara kwa mara hasa kupitia Facebook, Wema alikuwa akimueleza jinsi uhusiano wake na Chazz Baba ulivyo na changamoto huku Diamond akimfaraji, hilo likawafanya kuwa karibu na aliporudia wakaanza kuishi pamoja.

Ikumbukwe huu ulikuwa uhusiano mwingine kwa Wema ukimhusisha na staa kutoka tasnia ya burudani Bongo baada ya kuachana na Mr. Blue, TID na Chazz Baba ambaye baadaye walimaliza tofauti zao hadi kuhudhuria harusi yake!.

Uhusiano wa Wema na Diamond ukachukua nafasi wakiishi pamoja kama mume na mke kwa zaidi ya mwaka mmoja. Siku moja wakiwa ndani ya ndege Diamond akamwandikiwa Wema wimbo wenye ujumbe mzuri kwa penzi lao.

Wimbo huo ni Lala Salama (2012) uliobeba jina la albamu ya pili ya Diamond iliyotoka na nyimbo 10, hivyo tunaweza kusema Wema alikuwa na mchango wake katika mradi huu uliofanya vizuri.

Miongoni mwa nyimbo zinazopatikana katika albamu hiyo ni Mawazo (2012), kulingana na Wema wakati akiongea na Jarida la Mzuka 2013, wakati Diamond anaaza kushuti video ya wimbo huo chini ya Visual Lab: Next Level ndipo waliachana kwa mara ya kwanza.

Hiyo ni baada ya Wema kupata tetesi zilizodai kuwa Diamond ana uhusiano na Miss Tanzania namba mbili 2006, Jokate Mwegelo ambaye pia alitokea katika video hiyo pamoja na Hamisa Mobetto, Miss XXL After School Bash 2010.

Kitendo cha kuachana na kurudiana pamoja na mambo mengine yaliyofanya uhusiano wao kujadiliwa, vilipelekea Diamond kuwa mbunifu katika utunzi wa nyimbo zake kama Nimpende Nani (2012) aliyoelezea jinsi mapenzi yanamuweka njia panda.

“Yasiwe kama ya Wema Sepetu kila siku magazeti, ajue nidhamu na mila ya kwetu mjuzi kupetipeti…. Mpole kama Jokate, ila sauti kama Wema akiwa analia kicheko kama cha Fetty,” anaimba Diamond katika wimbo huo uliotengenezwa na KGT.

Wema ana historia kubwa katika muziki wa Diamond, ndiye mrembo aliyetajwa mara nyingi zaidi katika nyimbo za mwanamuziki huyo wa WCB Wasafi, ukiachana na Nimpende Nani (2012), nyingine ni Kesho (2012) na Fire (2017) akimshirikisha Tiwa Savage wa Nigeria.

Utakumbuka pia Wema alitokea katika video ya wimbo wa Diamond, Moyo Wangu (2012), na huo ukawa mwanzo kwa msanii huyo kuwatumia wapenzi wake katika video za nyimbo zake kitu kilichokuja kuigwa na wasanii wengi hapo baadaye hadi sasa.

Hata alipokuja kuwa na Zari The Bosslady, aliendelea na utamaduni huo, Zari ameonekana katika video mbili za Diamond, Utanipenda (2015) na Iyena (2018) ikiwa ni sawa na Hamisa aliyetoka katika video za nyimbo kama Mawazo (2012) na Salome (2016).

Mrembo mwingine ambaye hakuwa na uhusiano na Diamond lakini amepata bahati ya kuonekana katika video zake mbili, ni Malaika Salatis kutokea kisiwa cha Reunion ambacho kipo mashariki mwa Madagascar na Kusini Magharibi mwa Mauritius.

Huyu Malaika ndiye amecheza sehemu kubwa katika video ya Diamond, Jeje (2020) iliyotazamwa zaidi YouTube Afrika kwa mwaka huo ikitazamwa zaidi ya mara milioni 40, pia alionekana katika video ya wimbo, Gidi (2022) chini ya mradi wa Global Spin.

Utamaduni huo wa Diamond kuwatumia wapenzi wake katika video za nyimbo zake aliurithisha hadi kwa wasanii wa lebo yake ya WCB.

Harmonize alifanya video mbili na aliyekuwa mkewe Sarah, pia alifanya na wapenzi wake wengine, Jacqueline Wolper na Kajala Masanja, huku Rayvanny hadi sasa akiwa ameshatoa video sita na mpenzi wake Fahyma, na moja na aliyekuwa mpenzi wake, Paula.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *