Waziri wa Sheria alaani vikwazo visivyo vya kiadilifu vya Marekani na Magharibi dhidi ya Iran

Waziri wa Sheria wa Iran amelaani vikwazo visivyo vya kiadilifu vya Marekani na nchi za Magharibi kwa ujumla dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Amin Hossein Rahimi amelaani vikkwazo hivyo katika kikao na Mjumbe Maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayehusika na masuala ya ukatili dhidi ya watoto Dr Najat Maalla M’jid na kuongeza kuwa, watoto wa Kiirani wamekuwa wahanga wa vita, uvamizi na vikwazo visivyo vya kiadilifu vya Marekani na washirika wake, na kwa mwaka idadi ya watoto wa Iran wanaougua magonjwa kama vile saratani, thalassemia au ugonjwa wa kipepeo huaga dunia kwa sababu tu ya vikwazo visivyo vya kiadilifu vinavyokwamisha upatikanaji wa dawa za matibabu. 

Rahimi amekosoa hatua za undumakuwili za nchi za Magharibi kuhusu ukatili dhidi ya watoto na kusema misimamo hiyo ya Magharibi ni chanzo cha sintofahamu, ukosefu wa usawa na usalama kwa watoto. 

Mkutano wa Kimataifa wa Kukomesha Ukatili Dhidi ya Watoto ulifanyika tarehe 7 na 8 mwezi huu wa Novemba huko Bogota mji mkuu wa Colombia kwa ubunifu na kwa kuungwa mkono na Shirika la  UNICEF, Shirika la Afya Duniani (WHO), Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na Uswisi.