Naibu Waziri wa Fedha wa Russia Ivan Chebeskov amesema kitendo cha kuchukua riba inayopatikana kwenye mali zilizouiliwa za nchi hiyo ili kuipatia mikopo kwa Ukraine ni kinyume cha sheria za kimataifa na kitakuwa na matokeo yasiyotarajiwa kwa nchi za Magharibi.
Akizungumza na waandishi wa habari pembeni ya mikutano ya kila mwaka ya bodi zinazosimamia Shirika la Kimataifa la Fedha IMF na Benki ya Dunia inayofanyika mjini Washington, Marekani, Chebeskov amesisitiza kwa kusema: “bila shaka yoyote, maamuzi haya yaliyochukuliwa na Marekani na Umoja wa Ulaya si halali, yanakinzana na misingi ya sheria za kimataifa na Mkataba wa Umoja wa Mataifa na yanakwenda kinyume na kila kitu kilichopo”.
Chebeskov ameviambia vyombo vya habari vya Russiai kwamba vitendo kama hivyo vitakuwa na “matokeo hasi ya kihistoria” kwa mfumo wa fedha wa kimataifa.

Mapema wiki hii, Rais wa Marekani Joe Biden alitangaza uamuzi wa kuipa Ukraine mkopo wa dola bilioni 20, kwa kutumia riba kutoka kwa mali za Russia zilizozuiliwa. Wakati huo huo, Bunge la Ulaya limeunga mkono kutolewa mkopo wa hadi yuro bilioni 35 (dola bilioni 38) kwa Kiev.
Marekani na Umoja wa Ulaya zimezuia mali za Benki Kuu ya Russia zenye thamani ya karibu dola bilioni 300 baada ya Russia kuanzisha operesheni maalumu ya kijeshi dhidi ya Ukraine Februari 2022. Zaidi ya theluthi mbili ya fedha hizo, ambazo ni karibu dola bilioni 213, zinazuiliwa katika jumba la malipo la Euroclear lenye makao yake makuu mjini Brussels…/