Waziri wa mrengo wa kulia wa Israel atoa wito wa kukalia kwa mabavu Gaza, kupunguza idadi ya wakazi wake hadi nusu

Waziri wa Fedha wa Israel anayejulikana kwa itikadi kali ametoa wito wa kukaliwa kwa mabavu eneo la Ukanda wa Gaza na kupunguza nusu ya wakazi wa eneo hilo la Palestina ambalo linaendelea kushuhudia mauaji ya kimbari ya jeshi la Israel kwa karibu miezi 14 sasa.

Bezalel Smotrich, ambaye ana historia ya kutoa kauli za kibaguzi dhidi ya Wapalestina, alitoa matamshi hayo yenye utata wakati wa mkutano wa kundi la walowezi wa Kizayuni la Baraza la Yesha, Jumatatu iliyopita.

“Tunaweza kuikalia Gaza kwa mabavu na kupunguza idadi ya watu wake hadi nusu ndani ya miaka miwili,” kupitia njia ya kuhimiza kile kinachoitwa “uhamiaji wa hiari,” alisema.

Waziri huyo mbaguzi pia ameutaka utawala wa Tel Aviv kutumia uhusiano wake mzuri na utawala unaokuja wa rais mteule wa Marekani, Donald Trump, kutekeleza mpango huo.

“Kuikalia kwa mabavu Gaza sio neno chafu,” alidai Bezalel Smotrich.

Bezalel Smotrich

Amesema iwapo mpango huo utafanikiwa unaweza pia kutekelezwa katika Ukingo wa Magharibi.

Mwezi uliopita, waziri huyo wa serikali ya kibaguzi ya Israel alihimiza kunyakuliwa kikamilifu eneo la Ukingo wa Magharibi na Ukanda wa Gaza, akisisitiza kwamba Israel inapaswa kutangaza waziwazi kuwa hakutakuwepo taifa la Palestina.