
Waziri wa Utamaduni na Mwongozo wa Kiislamu wa Iran, amesema kwamba Shahidi Hassan Nasrullah alikuwa shakhsia mwenye kutafakari na kuchambua mambo ipasavyo na kuongeza kuwa: Shahidi huyu wa daraja ya juu alikuwa ni mchanganyiko adimu wa uwezo wa fikra na kutenda.”
Sayyed Abbas Salehi, Waziri wa Utamaduni na Miongozo ya Kiislamu wa Iran ameyasema hayo katika mkutano wa kimataifa wa “Fikra za Nasruullah” na kuongeza: “Alikuwa ni mwanasiasa kamili kitaifa, kieneo na kimataifa na pia kamanda mkuu wa kijeshi wakati wa mashambulizi ya Israeli dhidi ya Lebanon.”
Akifafanua zaidi kuhusu namna ambayo Shahidi Nasrullah alikuwa shakhsia wa kitaifa wa Lebanon na pia shakhsia wa Kiislamu wa kimataifa, Salehi alisema: “Ni nadra sana kwa mtu kuwa na sifa zote hizo.”
Waziri wa Utamaduni na Miongozo ya Kiislamu wa Iran amesema: Shahidi Nasrullah alikuwa meneja wa kistratejia na meneja wa medani ya mapambano.”
Aidha Salehi amesema kwamba Shahidi Nasrullah alijua vyema vyombo vya habari na diplomasia ya umma na alitumia vyema nyenzo hizo , na kuongeza kuwa : Njia ya Sayyed Hassan Nasrullah na njia ya Hizbullah bado ni imara na thabiti.
Kongamano la Kimataifa la Kuwaenzi Viongozi wa Muqawama lililopewa jina la ‘Fikra ya Nasrullah’ lilifanyika jana hapa mjini Tehran na kuhudhuriwa na wanazuoni kutoka nchi 13, zikiwemo Lebanon, Iraq, Bahrain, Misri, Kuwait, Uturuki, India, Malaysia, Algeria na Tunisia.