Waziri wa Mifugo na Uvuvi ashinda kesi madai ya Sh1 bilioni

Dar es Salaam. Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi ameibuka mshindi katika kesi ya madai ya zaidi ya Sh1 bilioni iliyofunguliwa na mfanyabiashara wa jijini Dar es Salaam, Shenaz Halari baada ya maofisa wa wizara kukamata nyavu zake za uvuvi.

Hukumu dhidi ya kesi hiyo ambapo Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), aliunganishwa kama mdaiwa wa pili, imetolewa Februari 14, 2025 na Jaji Arnold Kirekiano wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa hati ya madai, mfanyabiashara huyo alieleza Februari 20, 2017 maofisa kadhaa wenye silaha wakijitambulisha ni maofisa uvuvi, waliingia katika eneo lake, kuvunja kontena na kuondoka na mifuko 146 yenye nyavu.

Alidai maofisa hao walichukua nyavu zenye thamani ya Sh422.9 milioni na kwenda kuzitupa Kituo cha Polisi Chang’ombe na kushindwa kumshtaki kuthibitisha nyavu hizo zilikuwa haramu.

Mfanyabiashara huyo alifungua kesi ya madai namba 173 ya mwaka 2023, akiomba wadai waamriwe kumlipa Sh422.9 milioni ambayo ni thamani ya nyavu, riba inayofikia Sh515.8 milioni na fidia ya uharibifu Sh100 milioni.

Wadaiwa katika shauri hilo, Waziri na AG, walipinga kufanya jambo lolote baya na kueleza waziri alibaini kampuni ya Imara Fish Net Company, iliingiza nchini kinyume cha sheria, zana za uvuvi zikiwa katika mifuko 133.

Wadaiwa walidai nyavu hizo zilikuwa chini ya inchi tatu zinazoruhusiwa na sheria na zilihifadhiwa kituo cha polisi, ikielezwa kuna kesi ya jinai inayomkabili mdai katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ikisubiri kusikilizwa.

Kesi ya mdai ilijengwa na shahidi mmoja, Shenaz Halari mwenyewe aliyeieleza mahakama kuwa mwaka 2017, maofisa uvuvi kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, walivamia ghala lake na kutaifisha nyavu za uvuvi.

Alipofuatilia mzigo huo, alikamatwa akituhumiwa kuhifadhi nyavu haramu ambazo ni chini ya inchi tatu, na zana hizo zenye thamani ya kati ya Sh400 milioni na Sh500 milioni, zilihifadhiwa Kituo cha Polisi Chang’ombe.

Alitoa nyaraka zinazohusu kesi ya jinai namba 86 ya mwaka 2017 iliyokuwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ikithibitisha Februari 20, 2017 maofisa wa polisi na uvuvi walifika katika ghala lake.

Alieleza haikuwa mara ya kwanza kushtakiwa kwa tuhuma za aina hiyo, katika kuthibitisha alitoa kama kielelezo, nakala ya hukumu ya kesi ya jinai namba moja ya mwaka 2010 na hati ya mashitaka ya kesi ya jinai namba 99 ya 2020.

Alieleza mashitaka aliyoyaeleza ama yaliondolewa mahakamani au kusitishwa naye akaachiwa huru. Mdai alieleza alipoachiwa alifuatilia mzigo Kituo cha Polisi Chang’ombe lakini hakuupata.

Aliiomba mahakama iamuru alipwe fidia ya uharibifu anayodai ili aweze kuanzisha tena biashara, akieleza mzigo huo kukutwa kwenye ghala lake inathibitisha ni mali yake licha ya kutotoa nyaraka kuthibitisha.

Utetezi wa Serikali

Wadaiwa waliowakilishwa na mawakili wa Serikali, Pantaleo Urassa, Lilian Mirumbe na Salehe Manoro, waliita mashahidi wanne ambao ni Dickson Kasoki, Godfrey Banduka, Palaha Bulongo na Mrakibu Msaidizi wa Polisi, Juma Hebu.

Mashahidi hao walieleza Februari 20, 2017, ASP Hebu akiongozana na maofisa wengine akiwamo Banduka na Palaha, walifanya upekuzi na kukamata nyavu haramu zilizokuwa chini ya inchi 2.5 ambazo ni chini ya inchi tatu.

Kazi hiyo ilifanywa katika ghala linalomilikiwa na Imara Fishing Net Company lililopo Chamazi na kwamba, mdai hakuwa amesajiliwa na Wizara ya Mifugo na Uvuvi kama mfanyabiashara wa nyavu za uvuvi Tanzania.

Uamuzi wa mahakama

Jaji Kirekiano alisema madai ya msingi ya mfanyabiashara huyo ni kuwa wadaiwa walitaifisha nyavu zake halali za uvuvi ambazo zilikuwa kwenye kontena na kwenda kuzitupa Kituo cha Polisi Chang’ombe.

Jaji alisema amezingatia hoja isiyobishaniwa kuwa wadaiwa wana mamlaka ya kusimamia utekelezaji wa sheria ya uagizaji, uhifadhi na matumizi ya nyavu za uvuvi na kwamba, ili zana hizo ziwe halali, lazima zizingatie sheria za nchi.

“Wakati haibishaniwi kuwa wadaiwa walikamata nyavu hizo, wadaiwa wanasema zilikuwa chini ya ukubwa wa inchi tatu unaoruhusiwa kisheria na nyavu walizozikamata zilikuwa ni mali ya Imara Fish Net,” alisema na kuongeza:

“Ni muhimu kuzingatia kuwa mdai katika shauri hili anawajibika kuthibitisha kesi yake kwa viwango vinavyokubalika. Nimezingatia madai ya mdai na ushahidi kuwa ukamataji ule ulikuwa haramu kwa vile tu kesi dhidi yake ilisitishwa.”

Jaji alisema: “Wakati wa utetezi, wakili Rweshabura alimbana shahidi wa pili aeleze hatima ya kesi za jinai zilizofunguliwa dhidi ya mdai, lakini shahidi huyo aliamua kukaa kimya juu ya swali hili. Hii kaikuathiri kesi ya wadaiwa dhidi ya mdai.

“Baada ya mdai kueleza kuwa mashitaka ya jinai dhidi yake yalifutwa na kufuatia wadaiwa katika utetezi wao wa maandishi kueleza kesi hiyo bado iko Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, ulikuwa wajibu wa mdai kuthibitisha upande wake. Hakuna msingi wowote kusema ukamataji ule wa nyavu ulikuwa haramu.”

Jaji alisema hoja ya pili ambayo inapaswa kuamuliwa na mahakama ni kama mdai katika shauri hilo alikuwa na mamlaka ya kushtaki.

Jaji alisema kwa kusoma hati ya madai, ni wazi kuwa hoja ya nani ni mmiliki wa mzigo uliokamatwa inajitokeza, kwanza inaonyesha mmiliki wa mzigo ni kampuni ya Imara Fishnet Co Ltd, hivyo mdai hawezi kushitaki kwa kutumia jina lake binafsi.

Upande wa pili kwa mujibu wa jaji ni kuwa, kama mdai ndiye mmiliki wa mzigo uliokamatwa na alikuwa anaumiliki kwa jina lake, basi alipaswa kuthibitisha kuwa yeye ndiye mmiliki wa nyavu hizo na si kampuni ya Imara Fishnet.

“Kwa kusoma hati ya madai, inaonekana mdai anajitokeza kama ndiye mmiliki wa mali ileile tena kwa jina lake binafsi. Lakini ukitizama upande wa pili, alipopeleka kusudio la kushitaki alitumia jina la kampuni Imara Fishnet Company,” alisema.

Jaji alisema mdai alieleza kuwa mzigo ulichukuliwa kutoka kwenye ghala la kampuni ya Imara Fishnet Company na wadaiwa wakasema walichukua kutoka katika ghala hilo, ulikuwa wajibu wa mdai kuthibitisha umiliki.

Alisema kukosekana kwa ushahidi kuthibitisha mzigo ulikuwa ni wake binafsi na si wa kampuni, basi mzigo ulikuwa wa kampuni ya Imara Fishnet Company, hivyo mdai asingeweza kushitaki kama yeye kwa jina lake.

Kutokana na uchambuzi huo, aliitupilia mbali kesi hiyo na madai yote yaliyokuwa yameambatana nayo. Aliamuru mfanyabishara kulipa gharama za kesi baada ya kushindwa kuthibitisha madai yake.