
Waziri wa Mambo ya Nje wa Sudan, Ali Youssef, ametoa wito wa kufanyika “mazungumzo baina ya makundi yote ya Wasudani ambayo yatashirikisha mirengo yote ya kisiasa ili kumaliza vita vya ndani.”
Ali Youssef amesema katika mahojiano na televisheni ya Al Jazeera kwamba Wasudani wote lazima wasimame pamoja katika kukabiliana na changamoto za sasa, akisisitiza kuwa, “Wajibu wetu unatuhitaji kutetea nchi yetu na taasisi zetu katika kipindi hiki hii nyeti.”
Amesisitiza kwamba vita na kundi la Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF) vilitwishwa kwa jeshi la Sudan, na kwamba nchi hiyo inapinga uingiliaji wowote wa kimataifa katika mgogoro wa sasa Sudan. Amesema kwamba Wasudan “hawatakubali kuona kundi la RSF likiwa na mustakabali wowote wa kisiasa au kijeshi nchini humo.
Kuhusu mchakato wa mazungumzo ya kisiasa, Youssef amesema Khartoum ingali inashikamana na jukwaa la Jeddah kwa ajili ya kutatua mzozo wa Sudan, na wanamgambo wa RSF lazima watekeleze matokeo ya mazungumzo hayo, akielezea kwamba: “Mkataba wa Jeddah unahitaji waangalizi kuhakikisha utekelezaji wake, lakini tunapinga uingiliaji kati wa vikosi vyovyote vya majeshi ya kimataifa nchini Sudan.”
Tangu katikati ya Aprili 2023, Vikosi vya Wanajeshi vya Sudan (SAF) na Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF) vinapigana katika vita angamizi vya uchu wa madaraka na vimeshasababisha vifo vya zaidi ya Wasudan 20,000 na zaidi ya milioni 10 wengine kukimbia makazi yao.