
Dar es Salaam. Mwanamke wa kwanza kushika wadhifa wa uwaziri katika Baraza la mawaziri la Tanzania, Tabitha Siwale (86) amefariki dunia.
Dk Maka Siwale, mtoto wa marehemu akizungumza na Mwananchi leo Machi 13, 2025, amesema mama yake amefariki dunia usiku wa kuamkia leo akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Hindu Mandal.
Amesema mama yake aliyekuwa akisumbuliwa na maradhi ya utu uzima wanatarajia kumzika katika makaburi ya Kinondoni, Dar es Salaam, Jumamosi Machi 15.
Dk Maka amesema msiba upo nyumbani kwa marehemu Mikocheni kwa Nyerere.
Siwale aliyezaliwa mwaka 1939 mkoani Mbeya, alikuwa mwanamke wa kwanza kuwa waziri katika Serikali ya awamu ya kwanza ya Mwalimu Julius Nyerere. Alishika wadhifa huo mwaka 1975 akiwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.
Baadaye alihamishiwa Wizara ya Elimu akishika wadhifa wa Waziri. Aliapishwa na Mwalimu Nyerere kushika wadhifa huo Januari 15, 1980 katika Ikulu ya Dar es Salaam.
Siwale alichukua nafasi ya Nicholas Kuhanga aliyeteuliwa kuwa Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).
Hata hivyo, mwaka 1982 alirudishwa tena Wizara ya Ardhi hadi 1984 alipostaafu na kubaki kuwa mbunge hadi mwaka 2000.
Mbali ya hayo, aliwahi kuwa mwenyekiti na mjumbe wa bodi nyingi nchini. Pia alikuwa muasisi wa chama cha ushirika cha akiba na mikopo cha WAT.
Aliwahi kuwa mkuu wa shule mbalimbali za sekondari nchini zikiwamo za wasichana za Bwiru na Korogwe.
Mwaka 2000 alitunukiwa tuzo ya Mwanamke wa Karne na taasisi kutoka Marekani kutokana na mchango wake kwa Tanzania.