Waziri wa Jihad ya Kilimo wa Iran ametangaza kuwa ushirikiano kati ya Iran na Tanzania utaendelezwa katika nyanja za kilimo, petrokemikali na utalii.
Gholamreza Nouri Ghezeljeh amesema katika Tume ya Tano ya Pamoja ya Kiuchumi ya Iran na Tanzania kwamba: Kikao cha tume hii ya pamoja kitafanyika kesho Jumamosi baada ya miaka kadhaa ya kuahirishwa, na maandalizi tayari yamefanywa.
Waziri wa Jihad ya Kilimo wa Iran ameongeza kuwa: Hati 11 zimetayarishwa katika maeneo tofauti ya sekta ya umma na binafsi, na zitatiwa saini kesho katika kamisheni ya pamoja ya Iran na Tanzania.
Nouri Ghezeljeh amesema: Leo tumekuwa na kikao na Rais wa Zanzibar, Mhe. Dk. Hussein Ali Mwinyi kwa ajili ya kuchunguza nyanja za ushirikiano wa kiuchumi na kiutamaduni.
Amesema: Kwa kuzingatia historia ya uhusiano kati ya Iran, Zanzibar na Tanzania kwa ujumla, kuna nyanja nyingi nzuri za kuimarisha uhusiano huo.

Waziri wa Jihad ya Kilimo ameendelea kusema: Kwa msingi huo suala hili limetiliwa mkazo katika hati za ushirikiano katika nyanja za utamaduni na utalii, sayansi na uhawilishaji maarifa, usambazaji wa nyenzo zinazohitajiwa na nchi mbili, zikiwemo pembejeo za mifugo na nyenzo zinazohitajika katika tasnia ya ufugaji, pamoja na baadhi ya vyakula, bidhaa za kitropiki na viungo.
Amesisitiza kuwa, “nchi yetu inaweza kusaidia katika nyanja za gesi, petrokemikali, kilimo na uhawilishaji wa elimu na maarifa, na katika sekta za sayansi na utamaduni vinavyohitajiwa na na Tanzania’.