Waziri wa Utamaduni wa Croatia ametoa wito wa kuitumia tajiriba na uzoefu wa wafuasi wa dini tofauti nchini Iran katika kustawisha utamaduni wa kuishi pamoja kwa amani na masikilizano watu wa dini mbalimbali.
Nina Obuljen Koržinek ameeleza hayo katika kikao cha tatu cha mazungumzo baina ya dini mbalimbali na kubainisha kuwa, baadhi ya watu wenye misimamo ya kufurutu mpaka huwa sababu ya kuenea chuki na upinzani dhidi ya shughuli za kidini.
Koržinek ameongeza kuwa, baadhi ya watu wenye ushawishi huchochea tofauti na mifarakano kwa maslahi yao binafsi.

Waziri wa Utamaduni wa Croatia amesisitiza kwamba, katika hali hiyo, mazungumzo kati ya dini mbalimbali yanakuwa na umuhimu maradufu na kufafanua kuwa, mazungumzo na majadiliano yanaweza kutatua sutafahamu na hali ya kutoelewana; na ni kwa sababu hiyo Croatia inataka kuandaliwe mazingira ya kuwepo tamaduni kadhaa na dini mbalimbali ulimwenguni.
Duru ya tatu ya mazungumzo ya kidini kati ya Kituo cha Mazungumzo Baina ya Dini na Tamaduni Mbalimbali cha Shirika la Utamaduni na Mawasiliano ya Kiislamu la Iran na wanafikra wa kidini wa Croatia inafanyika katika mji mkuu wa nchi hiyo Zagreb, kwa kuhudhuriwa pia na Mohammad Mehdi Imanipour, Mkuu wa Baraza la Iran la Utungaji Sera na Uratibu wa Mazungumzo Baina ya Dini Mbalimbali.
Mada kuu ya duru hii ya mazungumzo ambayo yameandaliwa na Baraza la Dini la Croatia na kusimamiwa na Jumuiya ya Kiislamu ya Croatia, imetajwa kuwa ni “Tajiriba Zilizopatikana Katika Mazungumzo Baina ya Dini Mbalimbali”…/