
Dodoma. Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, amewasimamisha kazi watumishi wa mizani waliokuwa zamu katika mizani kutoka Tunduma, Mkoa wa Songwe, hadi Vigwaza mkoani Pwani, ili kupisha uchunguzi.
Agizo hilo limetolewa leo, Alhamisi Machi 20, 2025, na Waziri Ulega, ambaye ameunda pia ametangaza timu ya wataalamu kuchunguza tuhuma zinazowagusa watumishi hao waliokuwa zamu Machi 13, 2025.
Hatua hiyo imekuja baada ya kusambaa picha mjongeo katika mitandao ya kijamii ikimuonesha dereva aliyetambulika kwa jina moja la Pamela akilalamikia kunyanyaswa katika mzani wa Vigwaza.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma, Waziri Ulega amesema hatua hizo zimechukuliwa baada ya yeye kushauriana na menejimenti pamoja na wataalamu kutokana na malalamiko ya Pamela, aliyekuwa akiendesha lori la mzigo lenye tela, kuhusu tabia na maneno ambayo ameyaita ya udhalilishaji dhidi yake.
“Sasa, baada ya kufanya utaratibu wa kusikiliza kile ambacho alikilalamikia, nilitoa maelekezo kwa wataalamu wangu kupitia Katibu Mkuu kunipatia taarifa kuhusu kadhia ile. Niseme baada ya kupata taarifa ile, inanionyesha zipo sintofahamu ambazo zilijitokeza kutokana na jambo hili,” amesema.
Amesema kwa kusikiliza pande mbili hizo, unagundua kuna tatizo liko wazi ambalo limesababisha kuchukuliwa kwa uamuzi huo.
Amesema baada ya kugundua kuna tatizo, amemweleza Katibu Mkuu (Balozi Aisha Amour) kuwasimamisha kazi wasimamizi wa mizani wa barabara nzima, kuanzia Tunduma hadi Vigwaza.
“Nimeamua kutoa maelekezo ya kuwasimamisha wote waliokuwa katika zamu wakati tukio hilo linatokea. Tumefanya hivyo kwa lengo la kufanya uchunguzi, na tumeshaunda timu ya uchunguzi,” amesema Ulega.
Amesema timu hiyo itafanya uchunguzi kuanzia mahali ambapo lori hilo limeingia nchini hadi kufika mizani ya Vigwaza lilipotokea tukio hilo.
Ulega amesema ili kuwa na uchunguzi huru wa mwenendo wa tukio hilo, watachunguza pia malalamiko na mambo mengine yanayoendelea kwenye mizani nchini.
Kwa mujibu wa Ulega, timu hiyo itahusisha maofisa wa Serikali, ambao anaamini kuwa watafanya kazi kwa haki na kwa weledi mkubwa.
“Hii timu pia inaweza kutuletea mapendekezo mengine, na hatua zaidi za kinidhamu zitachukuliwa dhidi watakaobainika wamefanya ama wamekuwa na vitendo visivyoridhisha,” amesema.
Amesema kwa kuwa tatizo hilo ni la kujirudiarudia kwa miaka nenda rudi, hali iliyosababisha mtazamo wa Watanzania kuhusu mizani kuwa hasi, ameamua kuchukua hatua madhubuti.
Ulega amesema mizani zinaendeshwa na wanadamu, hivyo mambo yamekuwa mengi, ikiwemo lugha mbaya na baadhi ya watumishi kulalamikiwa kwa vitendo vya rushwa.
Amesema kutokana na hilo, amewaagiza Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) kubadilisha mifumo ya uendeshaji wa mizani nchini kwa kuwatangazia watu matumizi ya teknolojia badala ya watu kujadiliana.
Amesema mkakati wa muda mrefu ni kuhakikisha mizani zote 78 zinaendeshwa kwa mfumo wa kidijitali ambao, utapunguza mwingiliano kati ya watu kwenye maeneo hayo.
“Tunataka dereva akifika awe anaongea na mifumo na mashine, na mifumo isomane kwamba kila kituo na kituo kiwe na mawasiliano ya kimfumo. Jambo hili Rais Samia Suluhu Hassan amekuwa akisisitiza kuwe na mifumo inayosomana,” amesema.
“Mameneja ni lazima wawe wasimamizi wa mizani zetu zote hivi… Lakini hapo mbele tutaanza mara moja kuchukua hatua kwa mizani zitakazolalamikiwa, na mameneja tutawachukulia hatua pia. Isiwe ni kwa ajili ya watu wanaosimamia tu. Kwa muda mrefu wamekuwa wakijiweka kando kusimamia hili,” amesema.
Tukio lenyewe
Katika picha mjongeo iliyosambaa kwenye mitandao ya kijamii, ilionesha dereva huyo wa magari makubwa ya mizigo, ambaye anafanya kazi kwenye Kampuni ya Simba Logistics, akizungumza na baadhi ya vyombo vya habari, akisimulia safari yake ya kuanzia DRC hadi anaingia Tanzania akiwa amepakia mzigo wa tani 32.
Amedai Machi 13, 2025, alifika katika mzani wa Vigwaza akiwa anatokea DRC, ambapo gari lake lilizuiliwa kwa madai kuwa limezidi uzito.
Amefafanua kuwa hakukubaliana na jambo hilo huku akiwaeleza kuwa amepita mizani zote na hakukuwa na shida. Hata hivyo, amedai kuwa baada ya kutoa majibu hayo, maofisa walianza kumnyanyasa, wakimtaka aache kuwafundisha kazi, na kuamuru lori hilo liingizwe kwenye eneo la maegesho huku akitakiwa kulipa faini ya Sh956,400.
“Wamenizuia bila huduma zozote hapa, nikamuita mwenye mali, akaja na akawaambia wapime ili alipe faini, wakasisitiza wao wapo sahihi. Nikahoji, ‘Kwa nini ni sahihi wakati mizani zingine zote nimepita bila tatizo kwa maana uzito wangu uko kwenye viwango vianavyotakiwa, lakini hapa kwenu kuna tatizo?’’ amehoji.
Kwa mujibu wa maelezo ya Pamela, safari yake ilianzia Mpemba ambako alipita vizuri, Makambako, Mikumi, Mikese lakini Vigwaza alizuiwa licha ya nyaraka za mizani hizo kuwa na kiwango sawa cha uzito.
‘’Nimeandika barua kwa mamlaka, nikaonekana mkaidi. Naomba Waziri (Ulega) atuangalie sisi madereva wa Tanzania; hatuthaminiki, tunadharaulika na watumishi wa mizani wamekuwa na mtandao wa kutufuatilia ili ‘tuyaongee’ nao. Je, ni haki?” amehoji.