
Dodoma. Sakata la ajira ndani ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) limechukua sura mpya baada ya Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Dk. Stergomena Tax kusema jeshi hilo, kwa mujibu wa Katiba: “Hupokea amri kutoka kwa Amiri Jeshi Mkuu na si vinginevyo.”
Waziri Tax amesema hayo ikiwa ni takribani wiki mbili zimepita tangu tangazo la ajira la JWTZ kuibua mvutano bungeni, ikitajwa kuwa chombo hicho kimekiuka maagizo ya Bunge kwa kuweka kigezo cha waombaji kupitia JKT.
Kutokana na hilo, Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson, ameiagiza Serikali kupeleka majibu bungeni kuhusu kwa nini wameweka tangazo linalokwenda kinyume na maazimio yaliyotolewa na Bunge.
Aprili 30, 2025, JWTZ kupitia kwa Kaimu Mkurugenzi wa Habari na Uhusiano, Kanali Gaudentius Ilonda, walitangaza nafasi za ajira kwa vijana wenye taaluma mbalimbali, lakini katika kipengele ‘f’ waliweka kigezo cha ulazima wa muhusika kuwa amepitia JKT kwa kujitolea au kwa mujibu wa sheria na kutunukiwa cheti.
Mei 8, 2025, Mbunge wa Mbozi (CCM), George Mwenisongole, aliomba mwongozo wa Spika akitaka kujua ni kwa namna gani JWTZ wamekiuka Azimio la Bunge kwenye nafasi hizo kwa kuweka kigezo cha JKT tena.
“Mheshimiwa Spika, mwaka jana nilisimama hapa na kuomba mwongozo wa Spika kuhusu kigezo cha kutaka watu wanaotaka kuajiriwa kwenye vyombo vya ulinzi lazima wawe wamepitia mafunzo ya JKT. Leo tena JWTZ wamerudia kwenye mambo hayo, naomba mwongozo wako,” amesema Mwenisongole.
Spika Tulia alimsimamisha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Bunge, Sera na Uratibu, William Lukuvi, huku akimpa nakala ya tangazo hilo na Lukuvi alikiri kuwa Bunge lilipitisha Azimio hilo, lakini halikulenga moja kwa moja kwenye ajira za JWTZ.
“Hili linaleta ukakasi. Mbunge ameomba mwongozo, lakini tulishalipitisha hapa na Serikali ilikuwepo. Leo inapotolewa kigezo hiki kinakwenda kinyume na Azimio la Bunge. Kama chombo kinataka waajiriwa wake wapitie JKT, si wawaajiri halafu wawapeleke wenyewe JKT,” alisema Dk. Tulia.
Februari 16, 2024, Mwenisongole aliibua hoja wakati kulikuwa na tangazo la nafasi za ajira kwa vyombo mbalimbali vya ulinzi na usalama, ambapo baadhi waliweka kigezo cha wasailiwa kuwa wamepitia JKT na Jeshi la Kujenga Uchumi (JKU).
Katika hoja hiyo, kuliibuka mjadala mkali wa wabunge na mawaziri uliohitimishwa kwa Bunge kupitisha azimio la kuondoa kigezo cha kupitia mafunzo ya JKT na JKU.
Maelezo ya Waziri Tax
Leo Jumanne, Mei 20, 2025, Waziri Tax amewasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara yake kwa mwaka 2025/26 ya Sh3.64 trilioni, kati ya hizo Sh318.79 bilioni ni kwa ajili ya kugharamikia shughuli za maendeleo.
Bajeti hiyo, tofauti na nyingine, imepitishwa haraka kwani imekuwa na mchangiaji mmoja pekee ambaye pia ni Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Geofrey Pinda.
Akiwasilisha bajeti hiyo, Waziri Tax amegusia suala hilo la utaratibu wa kuandikishwa jeshini akisema kuwa, kulingana na Kifungu cha 3(2)(b) cha Sheria ya JKT, Sura 193 Toleo la Urekebishaji la Mwaka 2002, JKT linatakiwa kutoa mafunzo kwa vijana ili kuwawezesha kuwa na sifa za kuandikishwa katika Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).
Aidha, amesema Kifungu cha 29(1) cha Sheria ya Ulinzi wa Taifa, Sura 192 Toleo la Urekebishaji la Mwaka 2002, kinabainisha masharti kuwa mtu anaweza kuandikishwa JWTZ kwa kuzingatia masharti yatakayoelezwa kwenye Kanuni za Majeshi ya Ulinzi.
Amezitaja sifa za vijana kuandikishwa jeshini ambazo ni awe raia wa Tanzania, awe na tabia na mwenendo mzuri, awe na umri usiopungua miaka 18, awe na akili timamu na awe amekidhi vigezo vitakavyowekwa na Mkuu wa Majeshi kadri atakavyoona inafaa.
“Napenda pia kulitaarifu Bunge lako Tukufu kuwa marekebisho ya Sheria ya Ulinzi ya Taifa pamoja na Kanuni za Majeshi ya Ulinzi huidhinishwa na Rais na Amiri Jeshi Mkuu kwa ushauri wa Halmashauri ya Majeshi ya Ulinzi,” amesema.
Pia, Dk Tax amesema kulingana na Kifungu cha 148(1) cha Katiba ya Mwaka 1977 (kama ilivyofanyiwa marekebisho mara kwa mara), JWTZ hupokea amri kutoka kwa Amiri Jeshi Mkuu na si vinginevyo.
Amesema Kifungu cha 5 cha Sheria ya Ulinzi wa Taifa kinaainisha maeneo ambayo Waziri wa Ulinzi na JKT amekasimiwa mamlaka na Rais na Amiri Jeshi Mkuu.
Amesema tangu kuanzishwa kwake JWTZ Septemba mosi, 1964, limeendelea kutekeleza majukumu yake kwa umakini mkubwa, na kuwa hata pale palipotokea matishio, matishio hayo yalidhibitiwa ipasavyo na kwa wakati.
“Tukufu, natoa shukrani za dhati kwa Bunge, waheshimiwa wabunge na wananchi wote kwa kuendelea kuliamini na kulipa ushirikiano Jeshi letu. Kwa kutambua kuwa JWTZ ni chombo mahususi kwa shughuli mahususi ambazo zinahitaji weledi, umakini, na uzalendo wa hali ya juu,” amesema.
Ametoa rai kwa Watanzania kuendelea kuliamini na kuliwezesha JWTZ kutekeleza majukumu yake bila kuingiliwa, kwa kufuata matakwa ya Katiba, Sheria ya Ulinzi wa Taifa na kanuni zake, pamoja na sheria nyingine za nchi.
Ufafanuzi huo umekuja siku chache baada ya mjadala bungeni wa kutaka utaratibu wa kuandikisha jeshini kuondolewa sharti la kupitia katika mafunzo ya JKT.
Vipaumbele
Waziri Tax ameainisha maeneo ya vipaumbele 10, ikiwemo kuendelea kuiimarisha JWTZ kwa zana na vifaa vya kisasa na rasilimali watu.
Dk Tax amesema maeneo mengine ya vipaumbele katika mwaka 2025/26 ni kuendelea kuweka mazingira mazuri ya utendaji kazi ikiwemo stahili, makazi, mafunzo, matengenezo ya vifaa, na huduma bora za afya.
“Kuendelea kuimarisha miundombinu katika kambi, vikosi na shule za Jeshi na kuendelea kuimarisha uwezo wa Jeshi la Kujenga Taifa kwa kuboresha miundombinu ili liweze kuchukua vijana wengi zaidi,” amesema.
Waziri Tax ametaja maeneo mengine ni kuendelea kuimarisha Jeshi la Akiba, kuendelea kulinda miradi ya kimkakati kwa maslahi mapana ya Taifa na kushirikiana na mamlaka za kiraia kadri inavyohitajika.
Mengine ni kuimarisha mashirika na taasisi za utafiti wa masuala ya kijeshi, kuimarisha viwanda vya kijeshi (Defence Industries) na kuanzisha viwanda vipya kwa kushirikiana na sekta binafsi.
Vingine ni kuimarisha ushirikiano na Umoja wa Mataifa (UN), Umoja wa Afrika (AU), Jumuiya za Kikanda na nchi mbalimbali, na hivyo kuimarisha diplomasia ya ulinzi na kuendelea kutoa mafunzo ya ulinzi na stratejia.
Ametaja kipaumbele kingine ni kuendelea kuimarisha mifumo ya utawala bora na huduma kwa watumishi.
Utatuzi wa migogoro ya ardhi
Waziri Tax amesema kupitia Mpango wa Wizara wa Kutatua Migogoro ya Ardhi wa Mwaka 2020/21 – 2024/25, wizara imeendelea kutatua migogoro ya ardhi, ambapo migogoro yote inayojulikana imetatuliwa kwa kuhuisha mipaka, kupima maeneo, kufanya uthamini na kulipa fidia katika baadhi ya maeneo.
Amesema kwa mwaka wa fedha 2024/25, Sh15.34 bilioni zimetumika kama fidia kwa maeneo tisa ya vikosi, vyuo, shule na minara 17 katika mikoa tisa.
Amesema wamefanyia uthamini maeneo mbalimbali kati ya mwaka 2020/2021 hadi mwaka 2024/25 ambayo hayajalipwa na yako Hazina, yenye thamani ya Sh39.89 bilioni.
Ametaja maeneo hayo kuwa yako katika mikoa ya Songwe, Morogoro, Kigoma, Mwanza, Arusha, Dodoma, Pwani na Zanzibar.
Akichangia, Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Geofrey Pinda, amesema maeneo ya jeshi ni hatarishi kwa kuwa yanaacha baadhi ya mabaki ya vifaa vilivyotumika, ikiwemo mabaki ya mabomu.
“Tusipende kuyachezea maeneo haya kwa kuwa ni hatarishi. Niombe maeneo ambayo tumeainisha kuwa ni ya jeshi, wananchi tusipende kwenda kwa kuwa hayana matokeo mazuri kwa baadhi ya wananchi, kutokana na kuokota masalia ya mabomu na kuyachezea, yanaleta madhara,” amesema.
Maoni ya wabunge
Akiwasilisha maoni ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama, mjumbe wa kamati hiyo, Zahor Mohammed Haji, ameshauri wizara hiyo kuhakikisha inashirikiana na wizara nyingine kuweka mkakati wa pamoja kuhakikisha zinapatikana fedha za ununuzi wa vifaa tiba kwa ajili ya Hospitali ya Rufaa ya Kijeshi iliyopo Msalato, Dodoma.
Amezitaja wizara za kushirikiana kuwa ni Wizara ya Afya na Wizara ya Fedha, na kwamba kwa kufanya hivyo kutasaidia hospitali hiyo kuanza kutoa huduma kwa askari, maafisa na wananchi kwa ujumla.
Aidha, Haji ameshauri Wizara ya Ujenzi kushirikiana na Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa pamoja na Wizara ya Fedha, kwa pamoja kuandaa na kutekeleza mpango wa ujenzi na ukarabati wa barabara za kiusalama mipakani.
“Kufanya hivyo kutasaidia kuboresha barabara za kiusalama kuweza kupitika muda wote na hivyo kuimarisha ulinzi wa mipaka,” amesema Haji.
Akijibu hoja hiyo, Dk Tax amesema ameshakaa na mawaziri wenzake wanne na kufikia uamuzi wa kuliwekea mkakati mahususi suala la barabara za kiusalama na kuona jinsi ya kulimaliza.
Amewataja mawaziri hao kuwa ni Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Waziri wa Fedha, na Waziri wa Ujenzi.
“Tulichokifanya ni kuunda kamati itakayopitia vyanzo vyote vya fedha tulivyonavyo na kuona tunafanyaje ili kutatua changamoto hii ambayo imekuwa ni changamoto ya muda mrefu,” amesema.
Amesema kamati hiyo ya kitaasisi inatarajiwa kuwasilisha taarifa yake mwisho wa Mei 2025, na hivyo ana imani baada ya kupata taarifa wataona namna ya kutatua tatizo hilo la muda mrefu.