Waziri Silaa ataka vianzishwe vilabu vya kidijitali

Dar es Salaam. Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Jerry Silaa amezitaka shule na vyuo nchini kuanzisha vilabu vya kidijitali vitakavyosaidia kuongeza ujuzi wa teknolojia kwa wanafunzi.

Silaa amesema hayo leo Aprili 24, 2025 jijini Dar es Salaam kwenye kongamano kuadhimisha siku ya kimataifa ya wasichana katika Tehama lililoandaliwa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA). Limewakutanisha wanafunzi na wadau katika uga wa teknolojia.

Amesema klabu hizo zitakuwa mahususi kwa ajili ya kuwakutanisha wanafunzi katika ngazi mbalimbali za kielimu, kuhamasisha kusoma masomo ya sayansi na kujifunza teknolojia za kidijiti.

“Natoa wito kwa vyuo na shule za sekondari waanze vilabu vya kidijitali ili kuwahamasisha na kuwawezesha vijana kupata ujuzi wa teknolojia utakaowasaidia kuja na suluhisho la changamoto zinazoikabili jamii,” amesema.

Ametoa wito kwa wanafunzi wa kike nchini kuachana na dhana potofu kuwa masomo ya sayansi na teknolojia ni magumu na ni kwa ajili ya watoto wa kiume.

Silaa amesema masomo hayo ni kwa ajili ya wote bila kujali jinsia, akiwahimiza kuyasoma ili kupata ujuzi wa teknolojia utakaowawezesha kuja na bunifu zitakazosaidia jamii.

Ametoa wito kwa TCRA na mamlaka nyingine kuhakikisha bunifu za teknolojia zinazofanyika zinafikishwa kwa wadau husika ili ziweze kufikia hatua ya matumizi.

Waziri amesema Serikali imekuwa ikifanya jitihada kuhakikisha wananchi wanapata elimu ya teknolojia ya kidijiti inayowasaidia kurahisisha ufanyaji wa shughuli zao na kuwapatia kipato.

Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Dk Jabiri Bakari amesisitiza umuhimu wa kuwawezesha wasichana kupitia elimu ya kidijitali kama msingi wa maendeleo ya Taifa.

“Tushirikiane kwa pamoja kuwajengea uwezo wasichana katika teknolojia, hatua hii inaendana na ahadi zilizotolewa na nchi wanachama wa Umoja wa Kimataifa wa Mawasiliano (ITU) kukuza ushiriki wa wanawake katika taaluma zinazohusiana na teknolojia,” amesema.

Amesema TCRA inaunga mkono mpango wa kuanzisha vilabu vya kidijitali katika ngazi zote za elimu, kutoka shule za msingi hadi vyuo vya elimu ya juu.

“Vilabu hivi vitasaidia kuanza kuwajengea msingi wanafunzi hasa wa kike kupenda masomo ya sayansi na teknolojia,” amesema.

Millenium Antony, mhamasishaji wa wanawake katika masuala ya teknolojia amebainisha changamoto zinazowakabili ni pamoja na baadhi ya wanawake kuhisi hawana uwezo wa kutosha kuwa katika fani hiyo.

“Wanawake na wanaume wana uwezo sawa katika masuala ya teknolojia, hivyo wanawake pia wana uwezo wa kufanya mambo na kubuni vitu ambavyo vitakuwa msaada kwa jamii,” amesema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *