Waziri Mkuu wa Ireland: Tutawakamata Netanyahu na Gallant

Waziri Mkuu wa Ireland amesisitiza kuwa, nchi yake itatekeleza amri ya Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) kuhusu kukamatwa Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu na Yoav Gallant Waziri wa zamani wa vita wa utawala wa Kizayuni wa Israel.

Simon Harris amesisitiza kuwa, iwapo Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu ataingia Ireland, polisi watamkamata.

Waziri Mkuu huyo wa Ireland ameeleza kuwa, nchi hiyyo inaunga mkono maamuzi ya Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) na kwamba, itatekeleza kikamilifu agizo la mahakama hiyo la kutiwa mbaroni Netanyahu na aliyekuwa mshirika wake.

Hayo yanajiri katika hali ambayo, mataifa na shakhsia mbalinmbali ulimwenguni wameendelea kupongeza uamuzi wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) wa kutoa hati ya kukamatwa Waziri Mkuu wa utawala haramu wa Israel, Benjamin Netanyahu, na aliyekuwa waziri wake wa vita Yoav Gallant, wakituhumiwa kutenda jinai za vita.

Uswisi, Uholanzi na Ubelgiji sambamba na kupongeza uamuzi huo zimetangaza kuwa, zitamtia mbaroni Netanyahu endapo atakwenda katika mataifa hayo.

Waziri Mkuu wa Canada na Waziri wa Ulinzi wa Italia wamesifu uamuzi huo na kueleza kwamba, hiyo ni hatua ambayo wao walikuwa wakiitaka tangu awali.