
Haiti. Baraza la mpito la Rais la Haiti limemfukuza kazi Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Garry Conille aliyehudumu madarakani kwa miezi sita.
Kwa mujibu wa shirika la habari la United Press International (UPI), agizo hilo limetolewa leo Jumatatu, Novemba 11, 2024 na gazeti rasmi la Serikali Le Moniteur ambalo limemtaja Alix Didier Fils-Aime, (52) ambaye ni rais wa zamani wa Chemba ya Biashara Haiti kuteuliwa kuchukua nafasi ya Conille.
Agizo la kumtimua kazini Conille limeidhinishwa na wanachama wanane kati ya tisa wa baraza hilo. Hata hivyo, Conille amehoji uhalali wa agizo hilo akisema ingawa baraza lina mamlaka ya kuteua waziri mkuu, ni Bunge pekee lina mamlaka ya kumfukuza.
Haiti ni nchi yenye misukosuko na mara nyingi imekuwa ikikumbwa na machafuko ya wenyewe kwa wenyewe yanayoratibiwa na magenge ya wahalifu. Taifa hilo linakumbwa na ukosefu wa utawala tangu Rais Jovenel Moïse kuuawa Julai 2021, huku vurugu za magenge zikiendelea kuongezeka.
Katika barua yake, amesema kama waziri mkuu, zaidi kama raia wa Haiti, amechagua kwa uzalendo, kutokujibu hali hiyo kwa kugawanyika, bali kwa njia ya uwajibikaji.
“Bado ninaendelea kujitolea kufanya kazi kwa njia ya kujenga kwa ajili ya amani na utulivu katika nchi yetu na kusaidia juhudi zote za kurejesha amani na kuhakikisha utawala wa kidemokrasia, wazi na wa ushirikishaji.”
Conille aliteuliwa kuwa Waziri Mkuu wa Haiti Juni 2024 na baraza la mpito la wanachama tisa, ambalo lilianzishwa baada ya Waziri Mkuu, Ariel Henry kujiuzulu kutokana na ghasia za magenge kutawala mji mkuu wa Port-au-Prince.
Hata hivyo, Conille (58), alitegemewa kufanya kazi na baraza hilo kuelekea kufanyika kwa uchaguzi wa urais mwakani.
Kwa mujibu wa ripoti ya Umoja wa Mataifa kuanzia mwishoni mwa Septemba, watu 2,661 wameuawa Haiti kutokana na kuongezeka kwa ghasia za magenge.
Baada ya kutangazwa kwa kufutwa kazi kwa Conille, Ubalozi wa Marekani mjini Port-au-Prince umetoa taarifa ukiwataka raia wake kuepuka kusafiri kwenda Haiti, kwani kuna ripoti za maandamano na machafuko ya kiraia yanayoweza kutokea wiki zijazo.
Ikumbukwe, baraza la mpito lilibuniwa Aprili, likipewa jukumu la kuchagua waziri mkuu mpya, pamoja na baraza la mawaziri kwa matumaini ya kutuliza hali kwenye taifa hilo la Caribbean.
Hata hivyo, baraza hilo limegubikwa na siasa pamoja na migogoro, huku baadhi ya wanachama wake wakituhumiwa kuhusika kwenye ufisadi mwezi uliopita.