Dar es Salaam. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema kutumia vijana wa Kitanzania kubuni na kutengeneza mifumo ya fedha ya kidijitali kunahakikisha upatikanaji wa bidhaa na huduma za kifedha zinazokidhi mahitaji halisi ya Mtanzania wa kawaida.
Majaliwa amesema hayo leo Jumatatu, Machi 3, 2025, wakati wa uzinduzi wa huduma za benki ya NBC kidijitali, ambapo amesisitiza kuwa kutumia wazawa kunatoa suluhisho halisi la kifedha kwa kila Mtanzania na hivyo kuvutia Watanzania wengi zaidi katika mfumo thabiti wa fedha.
“Ni jambo la faraja kubwa kusikia kuwa huduma hii ya aplikesheni ya NBC Kiganjani na huduma nyingine tunazozindua leo, zimetengenezwa na wataalamu wa ndani wa NBC, ambao ni vijana wa Kitanzania,” amesema Majaliwa.
Amesema hatua hii, mbali na kuonyesha ukuaji wa elimu yetu na kupunguza gharama za kutumia wataalamu wa nje, ikiwemo leseni za kimataifa, inadhihirisha utayari wa Benki ya NBC kuwaamini watendaji wake, hususan vijana, katika kubuni suluhisho za kuongeza tija, kupunguza gharama za uendeshaji, na kuboresha huduma kwa wateja wake.

“Hili ni hatua muhimu kwa mustakabali wa vijana wa Tanzania. Hongereni sana…niwapongeze sana vijana hawa (naomba wasimame) kwa juhudi zao. Taifa letu linahitaji nguvu kazi ya vijana wake katika kuleta maendeleo endelevu,” amesema Majaliwa.
Amesema ustadi wao umeisaidia benki na Taifa kuokoa gharama kubwa zilizotumika kwa wataalamu wa nje na malipo makubwa ya vibali na leseni za kimataifa.
Awali, akitoa maelezo ya utangulizi mbele ya Waziri Mkuu na wageni wengine waliohudhuria, Mkurugenzi Mtendaji wa NBC, Theobald Sabi, amesema kwa aplikesheni hiyo kubuniwa na Watanzania, benki hiyo imeokoa zaidi ya Sh3 bilioni.
“Aplikesheni yetu ya NBC Kiganjani imetengenezwa na wataalamu wa ndani, vijana wa Kitanzania ambao wamesoma hapa nchini. Kama sio wao, tungetumia zaidi ya Sh3 bilioni, lakini pia malipo ya mara kwa mara kwa ajili ya usimamizi wake,” amesema Sabi.
Kuhusu aplikesheni hiyo, Sabi amesema huduma hiyo iliyoboreshwa ya NBC Kiganjani na huduma ya NBC Lipa Kiganjani (Lipa namba ya NBC) zinalenga kuleta mapinduzi ya mfumo wa fedha nchini kwa manufaa ya Watanzania wote.
“Kupitia NBC Kiganjani, mteja anaweza kufungua akaunti ya benki moja kwa moja kupitia simu yake ya mkononi na kuitumia papo hapo, bila kulazimika kutembelea tawi la benki. Kwa wateja wenye akaunti za mishahara, NBC Kiganjani inatoa mikopo ya papo hapo,” amesema Sabi.
Aidha, katika hafla hiyo, Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba, amesema hatua ya benki hiyo ni muhimu katika kuimarisha ujumuishi wa kifedha na kukuza uchumi wa kidijitali, na kwamba Serikali itaendelea kushirikiana na sekta ya kifedha kuhakikisha kuwa huduma kama hizo zinawafikia wananchi wengi zaidi kwa ufanisi na usalama.
“Zaidi, niendelee kuwashukuru sana NBC kwa ufadhili wake kwenye masuala mbalimbali ya kijamii, ikiwemo sekta ya michezo, hususan kupitia mchango wake mkubwa katika kuboresha Ligi Kuu ya NBC. Hongereni sana,” amepongeza Dk Mwigulu.
Kwa upande wake, Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Sauda Msemo, amesema sekta ya fedha imeendelea kuwa na ustahimilivu na hivyo kuwezesha shughuli mbalimbali za kiuchumi kufanyika.
Naibu Gavana huyo ametoa wito kwa taasisi zote za kifedha zifuate viwango bora vya usalama wa mitandao na kugundua haraka pale panapotokea udanganyifu wa aina yoyote.