
Dar es Salaam. Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa amebainisha faida tano zilizopatikana moja kwa moja baada ya kuanza kushirikiana na sekta binafsi katika Bandari ya Dar es Salaam, ikiwemo ongezeko la mapato hadi kufikia Sh8.26 trilioni kutoka Sh7.87 trilioni kwa kipindi cha mwaka mmoja.
Pia kupungua kwa gharama za uendeshaji kwa asilimia 30, kupungua kwa muda wa meli kusubiri nangani wastani wa siku 46 hadi saba, kupungua muda wa kuhudumia meli za makasha gatini kutoka wastani wa siku 10 hadi tatu.
Vilevile kuongezeka kwa wastani wa shehena ya makasha inayohudumiwa kwa mwezi kutoka 17,000 hadi 25,000 ikiwa sawa na ongezeko la asilimia 47.
Manufaa hayo yanaelezwa huku ikikumbukwa, Oktoba 22, 2023 Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA) iliingia mkataba na Kampuni ya DP World ya Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) wa uendelezaji na uendeshaji gati namba sifuri hadi n tatu na gati namba nne hadi saba za Bandari ya Dar es Salaam kwa kipindi cha miaka 30 ili kuongeza ufanisi wake.
Profesa Mbarawa amebainisha manufaa hayo leo Alhamisi Mei 15, 2025 bungeni jijini Dodoma wakati akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara yake kwa mwaka 2025/26 ya Sh2.7 trilioni.
Amesema wawekezaji hao wamewezesha upatikanaji wa vifaa, mitambo ya kisasa na mifumo ya Tehama inayoendelea kuleta ufanisi katika uendeshaji wa shughuli za kibandari.
Profesa Mbarawa amesema kuongezeka kwa mapato hayo kunatokana na shughuli za kibandari zinazofanyika katika kipindi cha kuanzia Julai 2024 hadi kufikia Februari 2025, mapato yatokanayo na Kodi ya Forodha kutoka bandarini.
“Makusanyo yanayokusanywa yanayotokana na shughuli za kibandari yamefikia Sh8.26 trilioni ikiwa ni ongezeko la Sh1.18 trilioni. Ni makubwa ikilinganishwa na makusanyo ya jumla ya Sh7.8 trilioni yaliyokusanywa katika kipindi kama hicho kwa mwaka 2023/24,” amesema Profesa Mbarawa.
Amesema ushirikiano huo umepunguza gharama za uendeshaji katika Bandari ya Dar es Salaam, hadi kufikia Sh685.16 bilioni sawa na punguzo la asilimia 30 ikilinganishwa na Sh975.01 bilioni zilizotumika katika uendeshaji kipindi kama hicho kabla ya kushirikishwa kwa waendeshaji binafsi.
“Kupungua kwa muda wa kusubiri meli nangani kutoka wastani wa siku 46 hadi wastani wa siku saba kwa meli za mizigo mchanganyiko na kichele (Bulk cargo) pia kupungua kwa muda wa kuhudumia meli za makasha gatini kutoka wastani wa siku 10 hadi tatu,” amesema.
Kulingana na Profesa Mbarawa ametaja faida zingine ni kuongezeka kwa wastani wa shehena ya makasha inayohudumiwa kwa mwezi kutoka 17,000 hadi makasha 25,000 ikiwa sawa na ongezeko la asilimia 47.
“Pia kuongezeka kwa makusanyo ya mapato yasiyo ya kikodi yanayokusanywa na taasisi mbalimbali za umma zinazotoa huduma bandarini,” amesema.
Profesa Mbarawa amesema pamoja na kuleta faida pia imechochea shughuli nyingine za kiuchumi katika sekta mbalimbali kutokana na kuimarika kwa utoaji huduma na hivyo kuleta ufanisi stahiki.
“Hatua hii imeendelea kuiwezesha Bandari ya Dar es Salaam kuwa lango la kibiashara kikanda na kimataifa,” amesema.
Vilevile, ushirikishwaji huu umechangia kufikiwa mapema kwa lengo la mpango kabambe wa TPA wa miaka 20 (2021/45), ulioweka shabaha ya bandari zote nchini kuhudumia tani milioni 30 za shehena ifikapo mwaka 2029/30,” amesema.
Amesema matokeo ya uendeshaji wa bandari hadi kufikia Machi 2025 tayari ufanisi wa uhudumiaji wa shehena wa bandari zote nchini umefikia tani milioni 27.55 matarajio ya Serikali hadi kufikia mwisho wa mwaka wa fedha wa 2024/25, ni kutimiza lengo la kufikisha tani milioni 30.
Changamoto
Aidha, Profesa Mbarawa amesema mbali na mafanikio hayo, wizara hiyo katika utekelezaji wa majukumu yake kwa mwaka 2024/25 inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo mabadiliko ya tabianchi.
“Katika kipindi hiki cha utekelezaji, mabadiliko ya tabianchi yameendelea kutokea na kusababisha hali ya hewa kubadilika mara kwa mara na kusababisha uharibifu wa miundombinu ya uchukuzi, hususan ya reli,” amesema.
Katika kukabiliana na hilo, Profesa Mbarawa amesema wanaendelea kuimarisha huduma za hali ya hewa ikiwemo kufunga Rada na kuongeza mtandao wa vituo ili kuimarisha utoaji na matumizi sahihi ya taarifa za na tahadhari ya matukio ya hali mbaya ya hewa.
“Kufanya tafiti mbalimbali zitakazosaidia kubaini athari za mabadiliko ya hali ya hewa kwa ajili ya usanifu wa miundombinu stahiki,” amesema
Pia Profesa Mbarawa ametaja changamoto nyingine ni mdororo wa uchumi wa dunia unaoathiri shughuli za usafiri na usafirishaji nchini, kutokana na uhusiano uliopo kati ya huduma zitolewazo ndani na gharama za huduma hizo katika soko la dunia.
“Tumeendelea kuchukua tahadhari za athari za mdororo wa uchumi wa dunia kwa kuweka mikakati ya kukabiliana nazo pindi zinapotokea, ili kutoleta madhara zaidi katika huduma za usafiri na usafirishaji nchini,”amesema.
Profesa Mbarawa ameitaja changamoto nyingi ni mahitaji makubwa ya fedha za utekelezaji wa miradi.
“Miradi mingi ya uchukuzi kuhitaji fedha nyingi (capital intensive) katika utekelezaji wake. Mathalan, mradi wa SGR utagharimu takriban Sh23 trilioni hadi kukamilika kwake.
“Mkakati tuliochukua ni kuendelea kuhamasisha sekta binafsi kutekeleza baadhi ya miradi inayohitaji uwekezaji mkubwa na hivyo kupunguza gharama kwa Serikali.”
Aidha, Serikali imeendelea kuwahusisha washirika wa maendeleo katika utekelezaji wa baadhi ya miradi. Mathalan, katika mwaka wa fedha 2025/26 washirika walikubali kutoa fedha za utekelezaji wa baadhi ya miradi,” amesema.