
WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Prof. Palamagamba Kabudi ameufuta Uongozi wa Kamisheni ya Ngumi za Kulipwa Tanzania (TPBRC) baada ya uchunguzi wa tuhuma mbalimbali zilizowasilishwa na wadau wa mchezo wa ngumi.
Taarifa ya Wizara wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo imeeleza kuwa, Mei 8, 2024, wizara hiyo iliunda Kamati Maalum ya uchunguzi yenye jukumu la kuchunguza malalamiko hayo na kubaini ukweli wake.
Baada ya kamati kukamilisha uchunguzi iliwasilisha taarifa ya yaliyobainika kulingana na tuhuma zilizowasilishwa. Kamati ilijidhihirisha pasi na shaka kuwa uongozi ulikuwa na mapungufu ya kiutendaji.
Mapungufu yaliyobainika ni matumizi mabaya ya madaraka kinyume na Sheria za nchi, Katiba ya Kamisheni ya ngumi za kulipwa Tanzania ya mwaka 2018 pamoja na ukiukwaji wa misingi ya utawala bora na usimamizi wa rasilimali za kamisheni.
Pia matumizi mabaya ya fedha kinyume na Sheria za nchi, Katiba ya Kamisheni ya Ngumi za kulipwa Tanzania 2018 pamoja na kanuni za uwajibikaji na usimamizi wa rasilimali za kamisheni.
Kufuatia mapungufu hayo, Waziri Kabudi ameelekeza hatua zaidi za kisheria zichukuliwe dhidi ya viongozi walioondolewa madarakani, ili kuweka fundisho kwa viongozi wengine wa vyama na mashirikisho na michezo nchini.
Hata hivyo, Waziri Kabudi ametoa angalizo kwa viongozi wa vyama na mashirikisho mengine ya michezo nchini kuhakikisha wanazingatia utawala bora unaofuata misingi ya katiba, kulingana na taasisi zao na katika nyadhifa wanazoshikilia katika taasisi hizo.
Serikali kupitia wizara hiyo imeendelea kusisitiza kuwa macho na kutetea maslahi na mienendo bora itakayochochea ustawi wa michezo nchini.
Kufuatia adhabu hiyo, Mwenyekiti wa Chama cha Mabondia wa Kulipwa Tanzania (TPBA), Japhet Kaseba ameonekana kuridhishwa nayo akiamini imetolewa kwa maslahi mapana ya mchezo wa ngumi hapa nchini.
“Ni jambo zuri kwani tunataka mchezo wa ngumi usiwe na konakona, ukiangalia hivi sasa mchezo huu umekuwa ajira kwa vijana wengi hivyo unahitaji viongozi makini,” amesema kiongozi huyo.