Waziri Junior naye atimkia Ligi Kuu Iraq

Dar es Salaam. Mshambuliaji Waziri Junior ameachana na Dodoma Jiji na kujiunga na Al Mina inayoshiriki Ligi Kuu ya Iraq kwa mkataba wa miezi sita.

Junior ambaye ametua Al Minaa akitokea Dodoma Jiji FC inayoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara, anakuwa Mtanzania wa pili kucheza soka la kulipwa nchini humo akifuata nyayo za Saimon Msuva anayeichezea Al Talaba.

Katibu Mkuu wa Dodoma Jiji, Fortunatus Johnson alisema kuwa Waziri Junior atacheza hadi mwishoni mwa msimu ndani ya Al Minaa na baada ya hapo watajadili hatima yake msimu ukimalizika.

“Ameshaondoka tangu Februari 07. Yupo kwa mkopo baada ya miezi sita tutaangalia namna gani ya kuboresha maslahi ya nyota huyo.

“Timu hiyo ilimuona alipokwenda kufanya majaribio nchini Brunei ambako kulikuwa na mawakala mbalimbali. Baada ya timu ya nchi hiyo kuchelewa, Mina’a ikamsajili,” alisema Fortunatus.

Msimu wa 2015/16 na 2016/17 akiwa na Toto Africans alifunga mabao 14, msimu uliofuata akatua Azam FC na kufunga bao moja, msimu 2018/19 (Biashara United) mabao matatu.

Akiwa Mbao FC, Waziri Jr alifunga mabao 14 kwenye mechi 12 msimu 2019/20, ndipo Yanga ikamsajili msimu uliofuatia akafunga mabao mawili, 2021/22 mabao manne Dodoma Jiji akacheza misimu miwili KMC na kufunga mabao 13.

Msimu huu umeonekana kuwa mgumu kwa Waziri Junior ndani ya Dodoma Jiji kutokana na majeraha ya mara kwa mara ambayo yalikuwa yakimkabili huku pia akionekana kushindwa kumshawishi kocha Mecky Maxime kumpa nafasi katika kikosi cha kwanza.

Tegemeo kubwa la Dodoma Jiji msimu huu limekuwa mshambuliaji Paul Peter huku Maxime akitoa nafasi mara kadhaa kwa Daud Milandu au Reliants Lusajo.

Dodoma Jiji inashika nafasi ya 11 kwenye msimamo wa Ligi Kuu ikiwa imekusanya pointi 20, ikifunga mabao 18 na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara 24.