
Dar es Salaam. Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Selemani Jafo amewahimiza wabunifu ikiwemo sekta ya muziki kusajili kazi zao ili wapate faida, kuepuka migogoro sambamba na kukosa kipato.
Waziri Jafo amesema wabunifu hao wakisajili majina, maneno na chapa ‘brand’ itawawezesha kufanya kazi zao kwa kujiamini huku wakiwa na uhalali wa umiliki.
Ametoa kauli hiyo leo Jumatano Mei 21, 2025 jijini Dar es Salaam wakati Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), ikiadhimisha siku ya Miliki Ubunifu Duniani (World Intellectual Property Day).
Lengo la maadhimisho hayo yenye kauli mbiu isemayo “Miliki Ubunifu na Muziki: Sikilizia Mdundo wa Miliki Ubunifu”, ni kujadili fursa, mafanikio na changamoto zilizopo katika nyanja ya miliki, hususan tasnia ya muziki.
“Ukisajili utapata nguvu ya kisheria na haki ya kupata kipato ambayo utaitumia kwa muda wote hata vizazi vyako vitakuja kunufaika na kazi zako,” amesema Dk Jafo.
Katika kuhakikisha hilo ametoa agizo kwa taasisi ya Brela na nyingine kuendelea kutoa elimu ya usajili kwa wabunifu nchini ili wapate haki zao.
Kauli ya Dk Jafo inaungwa mkono na Ofisa Mtendaji Mkuu kutoka Brela, Godfrey Nyaisa aliyesema changamoto moja wapo inayowakabili wasanii ni kukosa uelewa wa suala zima la usajili wa kazi zao pamoja na umuhimu wa majina yao.
“Wanamuziki wengi hawaelewi kuwa chapa zao zinapaswa zisajiliwe, tunafanya jitihada lakini bado ma fanikio sio mazuri sana. Ndiyo maana tunawakutanisha ili wapate uelewa,” amesema.
Nyaisa amewasisitiza wasanii kulinda alama zao wanazotumia kama utambulisho katika kazi zao za muziki ili iwe kisheria, huku akitahadharisha mabadiliko ya sayansi na teknolojia yanazidi kuwa tishio pale maudhui yanaposambazwa bila idhini.
“Mfano umetolewa wasanii wa zamani kama Marijani Rajabu, Mbaraka Mwishehe tunaona kazi zao zinapigwa maeneo mbalimbali lakini hawapati chochote hata familia zao,” amesema.
Kwa upande wake, Kaimu Ofisa Mtendaji Mkuu Ofisi ya Hakimiliki Tanzania (Cosota) Philemon Kilaka amesema katika kutekeleza jukumu la usajili kuanzia mwaka 2001 hadi 2025 wamesajili wasanii 3,695 na kazi zao 32,000 za muziki zimesajiliwa.
Akitoa ushuhuda juu ya suala la elimu ya usajili msanii wa muziki, Farid Kubanda maarufu kama Fid Q, amesema changamoto moja wapo aliyowahi kukutana nayo ni kujaribu kuuza wimbo kwenye matumizi ya filamu ingawa hakujua mkataba aliopewa kama utatumiwa na matumizi mengine.