
Unguja. Mwaka mmoja tangu Bandari ya Dar es Salaam apewe mwekezaji DP World, imeelezwa kuwa mafanikio na mabadiliko makubwa yameanza kuonekana katika operesheni za kuhudumia makontena na kukuza mapato.
Oktoba 2023, Serikali iliingia mikataba mitatu ya uwekezaji na uendeshaji wa bandari hiyo na kampuni ya DP World kwa lengo la kuongeza ufanisi.
Kabla ya kutia saini, Serikali iliingia makubaliano na Serikali ya Dubai kuhusu uwekezaji huo (IGA), ambayo yalikosolewa na wadau mbalimbali. Hata hivyo, Serikali ilisisitiza kuwa mkataba huo utakuwa na manufaa makubwa.
Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari kuhusu mkutano wa kimataifa wa Shirikisho la Vyama vya Mawakala wa Forodha kisiwani hapa leo Jumatatu, Machi 10, 2025, Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, amesema tangu bandari hiyo apewe mwekezaji huyo, uhudumiaji wa makontena umeongezeka kutoka siku saba hadi siku mbili.
“Kwa ufupi, ufanisi wa Bandari ya Dar es Salaam umebadilika sana. Kwa mfano, meli za makontena zilikuwa zinakaa bandarini kwa siku saba, lakini sasa zinaingia ndani ya saa 24 au siku mbili na kuondoka. Yaani, kutoka siku saba hadi wastani wa siku mbili,” amesema Waziri Mbarawa.
Licha ya kueleza kuwa upande wa meli za shehena ya jumla (loose cargo) bado haujaonyesha ufanisi mkubwa, amesema hali imeboreshwa kwani hapo awali meli hizo zilikaa nangani kwa wiki mbili hadi tatu, lakini sasa zinakaa kwa siku tano.
Kuhusu mapato, amesema kuwa kati ya Aprili na Juni mwaka jana, walikusanya karibu Sh490 bilioni. Wanatarajia kufikia Juni mwaka huu, mapato ya bandari hiyo yatafikia Sh1.7 trilioni, kiwango ambacho hakijawahi kufikiwa. Hata hivyo, hakutaja kiwango cha awali kabla ya uwekezaji huo.
“Kwa hivyo, uwekezaji wa DP World pamoja na ule wa ndani umeleta mabadiliko katika Bandari ya Dar es Salaam. Zamani kontena zilikaa siku saba, lakini sasa zinatolewa ndani ya siku mbili,” amesema.
Kwa mujibu wa Waziri Mbarawa, kabla ya kuja kwa mwekezaji huyo, bandari ilikuwa inahudumia makontena 650,000 kwa mwaka, lakini sasa idadi hiyo imeongezeka hadi milioni 1.022.
“Zamani tulikuwa tunahangaika, lakini sasa ufanisi umeongezeka, huduma zimeboreshwa, na mapato pia yameongezeka. Tunamshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutengeneza mazingira mazuri ambayo yameleta mabadiliko,” amesema.
Wakati wa utiaji saini wa mkataba huo, Oktoba 22, 2023, Ikulu ya Chamwino, tukio hilo liliwashuhudiwa na Rais Samia Suluhu Hassan.