Waziri Aweso awatafutia fursa wahitimu Chuo cha Maji

Dar es Salaam. Waziri wa Maji, Jumaa Aweso amezitaka mamlaka na wakala wa maji kuwatumia wahitimu wa Chuo cha Maji kupunguza uhaba wa ajira.

Waziri amesema hayo leo Jumatano Novemba 13, 2024 katika mahafali ya 48 ya Chuo cha Maji yaliyofanyika jijini Dar es Salaam.

Waliohitimu ngazi ya cheti cha msingi cha ufundi 19, cheti cha ufundi 4, stashahada ya kawaida 457, stashahada ya juu mmoja na shahada 203 jumla wote 684.

Amesema chuo hicho kilianzishwa kwa ajili ya kusaidia wizara, hivyo wanatakiwa kutumika katika miradi ya mamlaka za maji.

Aweso amesema wananchi wanalalamika hawana maji lakini wakipita mitaani wanaona maji yanamwagika hiyo ni hasara kwa Taifa.

“Mamlaka za maji zipo lakini upotevu wa maji umeendelea na umekithiri hivyo wakafanye kazi ya kulinda maji,” amesema Aweso.

Amesema makandarasi wanakuwa na miradi zaidi ya 15 katika wilaya moja na hawezi kusimamia yote kwa wakati mmoja, ili kwenda na kasi amewataka kuchukuliwa kwa vijana waliohitimu kusimama.

“Mkandarasi akiondoka katika eneo la mradi anatakiwa kuacha mtu muaminifu ili kazi iendelee hivyo wakichukuliwa vijana kutapunguza uhaba wa watumishi na kusaidia kujifunza pindi mkandarasi mgeni anapoondoka,” amesema.

Mbali na hilo, Aweso ameagiza uongozi wa Wizara ya Maji kufanya kikao na Chuo cha Maji kwa ajili ya kufuatilia changamoto zilizopo na zile zinazohitajika kuchukuliwa hatua watafanya hivyo.

Kutokana na maelezo yaliyotolewa na Waziri Aweso kwa niaba ya viongozi wengine, Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji Handeni, Yohana Mgaza amesema watatekeleza maelekezo yaliyotolewa kwani wana miradi mingi hivyo watachukua vijana kutoka chuoni hapo.

“Unachokisema kwetu ni utekelezaji kwa hiyo tutafanya kama ulivyoagiza ya kuwachukua vijana kwenye miradi yetu kwa sababu tuna upungufu wa watumishi,” amesema Mgaza.

 Mkuu wa Chuo cha Maji, Dk Adam Karia amesema chuo hicho kimejipanga kukabili changamoto mbalimbali za sekta ya maji kwa kuendelea kuwafunza wataalamu katika sekta hiyo na kufanya utafiti utakaotumika kuondoa changamoto ya maji kwa Watanzania.

Pia, amesema chuo hicho kina jumla ya wafanyakazi 124 kwa sasa kati yao 73 ni wanataaluma na watumishi 51 ni utawala idadi ambayo haitoshi kwani bado chuo kinatumia walimu wa muda ‘part timers’ na wanahitaji watumishi 250.

Aidha, ameeleza kuhusu miundombinu chakavu ya majengo ikiwamo sehemu ya mikutano ya hadhara, hali iliyosababisha kutojipanua zaidi nakuongeza idadi ya wanafunzi.