Waziri atoa miezi mitatu wakulima, wafanyakazi kiwanda cha Chai Mufundi walipwe stahiki zao

Iringa. Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara nchini, Exaud Kigahe ametoa miezi mitatu kwa kampuni ya DL, inayoendesha kiwanda cha chai kilichopo Mufindi, kuhakikisha kuwa malipo ya wakulima na wafanyakazi wa kiwanda hicho yanakamilika kuanzia Aprili hadi Juni 2025.

Kauli hiyo ilitolewa jana, Aprili 5, 2025, katika mkutano uliofanyika nje ya kiwanda hicho cha chai kilichopo Wilaya ya Mufindi, mkoani Iringa, ambapo Waziri Kigahe alikutana na wakulima wa chai na wafanyakazi wa kiwanda hicho ili kujadili changamoto za malipo, hasa baada ya kiwanda kusimama kufanya kazi tangu Januari 28, 2025.

Wakulima wa chai na wafanyakazi wamesema kuwa wanakutana na hali ngumu ya kimaisha kutokana na kutolipwa stahiki zao kwa muda mrefu, hali inayosababisha baadhi yao kuacha kazi.

Baadhi ya Wakulima wa chai na wafanyakazi wa kiwanda cha chai Mufindi wakiwa nje ya kiwanda hicho wakimsikiliza Naibu Waziri wa viwanda na biashara nchini, Exaud Kigahe kuhusu madai yao wanayodai kuanzia Januari mpaka Machi, 2025.Picha na Christina Thobias.

Wafanyakazi hao, ambao ni nguzo muhimu katika uzalishaji wa chai, wamesema wamekuwa wakililia malipo yao bila mafanikio, na hali hiyo inaathiri familia zao na maisha yao.

Waziri Kigahe alisisitiza kuwa Serikali inatambua changamoto zinazowakabili wakulima na wafanyakazi hao, na ameiagiza kampuni ya DL kuhakikisha malipo yanafanyika kwa wakati ili kurudisha hali ya kawaida na kuendeleza shughuli za kiwanda hicho.

Naye Hamza Kanyika, Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi wa Kiwanda cha Chai Mufindi, ameeleza kuwa wafanyakazi wengi wanakosa morali wa kuendelea na kazi kutokana na kushindwa kulipwa stahiki zao kwa wakati.

“Tuliobaki hapa ni wenye moyo wa chuma, wengine wameshaacha kazi, na sasa ni mwezi wa tatu hatujalipwa chochote. Hapa nilipo, natamani kulia,” amesema Kanyika, akionyesha huzuni na hasira kutokana na hali hiyo inayowaathiri wafanyakazi na familia zao.

Baadhi ya Wakulima wa chai na wafanyakazi wa kiwanda cha chai Mufindi wakiwa nje ya kiwanda hicho wakimsikiliza Naibu Waziri wa viwanda na biashara nchini, Exaud Kigahe kuhusu madai yao wanayodai kuanzia Januari mpaka Machi, 2025.Picha na Christina Thobias.

Katika hatua nyingine, wafanyakazi hao wamesema kuwa wamekuwa wakifanya kazi bila malipo kwa miezi mitatu, hali inayowaweka katika mazingira magumu kiuchumi.

Wamelalamika kuwa familia zao zinapata shida kubwa kutokana na kutokuwa na fedha za kuendesha maisha ya kila siku, jambo linalowafanya kuwa katika hali ya wasiwasi mkubwa.

Kwa upande wa wakulima wa chai, wamesema kuwa wamekuwa wakilima kwa bidii kubwa, lakini licha ya juhudi zao, wamejikuta wakiishi katika umaskini kutokana na kushindwa kupata malipo ya haki kwa mazao yao.

“Hali yetu ni ngumu, tumekuwa tukilima chai kwa miaka mingi, lakini sasa tunaishi kwa matumaini kwani hatujapata fedha stahiki kwa muda mrefu,” amesema Jesca Ngimba, mmoja wa wakulima wa chai, ambaye alionyesha wasiwasi kuhusu kulipwa fedha zao.

Aidha, wakulima na wafanyakazi hao wameeleza kuwa kiongozi wa kiwanda hicho amekuwa akiahidi kulipa madeni yao, lakini ahadi hizo zimekuwa zikichelewa, hali inayoongeza hasira na malalamiko miongoni mwa wafanyakazi na wakulima.

Katika hatua nyingine, Waziri Kigahe, baada ya kuwasikiliza wakulima na wafanyakazi hao, ameeleza kuwa serikali inatilia mashaka kuhusu hali ya kiwanda hicho, huku akionyesha wasiwasi kwamba shamba la chai linaweza kugeuka kuwa pori kutokana na kushindwa kulipa wakulima wadogo na wafanyakazi wa kiwanda.

Waziri Kigahe amemuagiza Mkurugenzi Mwendeshaji wa kiwanda hicho, Jefferson Mofwi, kuhakikisha kila mfanyakazi anapewa stahiki zake, ikiwa ni pamoja na mafao ambayo hadi sasa yanadaiwa kufikia kiasi cha Sh1.6 bilioni.

Kwa upande wa wakulima, Waziri Kigahe ameagiza kuwa malipo ya fedha wanazodai, ambazo ni takribani Sh124 milioni, yalipwe kwa kipindi cha miezi mitatu kuanzia sasa.

“Wananchi wanashangaa kuona viongozi wa serikali wanaruhusu kiwanda chetu kife, wakati kilikuwa na umuhimu mkubwa kwetu. Nasisitiza kuwa kiwanda cha chai ni muhimu, na hiki ndicho kilichonisomesha,” ameongeza Waziri Kigahe.

Kwa mujibu wa Waziri Kigahe, Serikali imejipanga kuongeza juhudi katika kukuza viwanda nchini, ikiwa ni pamoja na kuanzisha viwanda vya BBT, ili kusaidia mchakato wa maendeleo na kuongeza ajira kwa wananchi wengi zaidi.

Akijibu madai ya wakulima na wafanyakazi hao, Mkurugenzi Mwendeshaji wa Kiwanda cha Chai cha Mufindi kutoka kampuni ya DL, Jefferson Mofwi, amewaomba radhi wakulima na wafanyakazi wa kiwanda hicho kutokana na ucheleweshaji wa malipo yao.

Alieleza kuwa kiwanda kimejizatiti kutatua changamoto hiyo, akisema kuwa sababu ya kutolipa kwa wakati ni kushuka kwa uzalishaji wa chai, tofauti na miaka mingine ambapo uzalishaji ulikuwa juu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *