Unguja. Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Saada Mkuya kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mapato Zanzibar (ZRA) wameanza operesheni mtaani ili kuwabaini na kuchukua hatua dhidi ya wafanyabiashara wanaokwepa kodi.
Mbali na sheria kuwataka wafanyabiashara kutoa risiti za kielektroniki na kubandika bei halisi za bidhaa husika, pia wamebainika kuwapo wafanyabiashara ambao hawabandiki bei hizo, ikitajwa kuwa sehemu ya mpango wa kuficha uhalisia wa utoaji wa risiti.
Katika operesheni iliyofanyika leo Jumatano, Machi 5, 2025, katika maeneo ya Mlandege kwenye maduka mbalimbali, Dk Saada amesema kama ni elimu, imeshatolewa, kilichobaki ni kuwachukulia hatua za kisheria.
Amesema wamebaini wafanyabiashara wanawaweka wafanyakazi madukani na kuwapa maelekezo kwamba wasitoe risiti, au zikitolewa, ziwe tofauti na bei walizonunulia bidhaa.
“Kama elimu imeshatolewa na inaendelea kutolewa, hatua iliyobaki sasa ni kuchukua hatua kwa mujibu wa sheria za kodi, kwani maduka mengi tumeyakuta yanakiuka sheria,” amesema.
Amesema Serikali itaendelea kusimamia na kutekeleza sheria za kodi kama zinavyoeleza ili kuwachukulia hatua wafanyabiashara ambao hawatoi risiti na wananchi ambao hawadai risiti wanapofanya manunuzi.

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Saada Mkuya akitoa maelekezo kwenye moja ya maduka alipofanya ukaguzi na kukuta hawatoi risiti za kielektroniki wala kubandika bei halisi kwenye bidhaa husika.
Kwa mujibu wa sheria za kodi, hususan za Ongezeko la Thamani (VAT), inamtaka mfanyabiashara anapouza bidhaa, bei ionekane wazi, lakini wengi wanakwepa kuweka bei.
Kwa mujibu wa sheria hiyo, mfanyabiashara anayekataa kutoa risiti ya kielektroniki, faini yake ni Sh2 milioni, na mwananchi ambaye ananunua bidhaa bila kudai risiti, faini yake ni Sh30,000 kwa kila bidhaa.
“Kitendo cha kutobandika bei za bidhaa ndicho mwanya wa kufanya udanganyifu. Mteja akienda kununua bidhaa, anaambiwa iwapo anataka risiti, ataandikiwa bei nyingine; kama hachukui risiti, pia anaandikiwa bei nyingine tena, punguzo tofauti na bei halisi aliyonunulia bidhaa,” amesema.
Waziri Saada amesema Serikali itachukua hatua, kwani imekuwa ni utaratibu kwa watu wanapotaka kujificha katika kigezo cha kulipa kodi, kutobandika bei za bidhaa wanazouza.
Naye Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Zanzibar (ZRA), Said Kiondo Athumani, amesema ZRA itaendelea kufanya kaguzi hizo kwenye maeneo yote yanayofanywa biashara, lengo likiwa kuwakumbusha wananchi na wafanyabiashara suala la kutoa risiti na kudai risiti ni lazima, siyo hiari.
Amesema wananchi lazima wafahamu kwamba wanapodai risiti ya malipo wanayoyafanya, wanakuwa wamelipa kodi, kinyume chake wanawanufaisha wafanyabiashara pekee.
“Ili kuhakikisha kodi yako imeingia katika mchango wa mapato ya nchi, basi dai risiti. Unapoidai, mifumo yetu itaona kwamba kitu kimenunuliwa na kiwango cha kodi kinachoingia kwenye mfuko mkuu wa Serikali. Tusikubali kuacha kudai risiti na fedha zetu kupotea mifukoni mwa wafanyabiashara,” amesema.
Amewasisitiza wafanyabiashara kushirikiana na ZRA katika kukusanya kodi na wasikubali kukimbizana, badala yake kila mmoja atimize wajibu wake kuhakikisha Serikali inapata mapato yake kama ilivyokusudia.
Kwa wafanyabiashara ambao wamebainika kufanya mauzo bila kutoa risiti kwa muda wa siku nne, Kamishna Kiondo amesema ZRA itahakikisha inawachukulia hatua za kisheria, ikiwemo kupiga penati na kutoza riba.
“Usingojee kuchukuliwa hatua za kisheria, bali wajibika mwenyewe na tetea maendeleo ya nchi yako ili kwa pamoja tuijenge Zanzibar yetu,” amesema.
Mmoja wa wafanyakazi katika duka la vyombo (jina lake limehifadhiwa) amesema wamekuwa wakipewa maelekezo na bosi wao, ambaye yupo nje ya nchi, kutotoa risiti.
Mmoja wa wafanyabiashara katika eneo hilo, Khamis Khamis, amekiri kutotoa risiti kama inavyoelekezwa, akisema kuna changamoto ya mtandao.
Kuhusu kutobandika bei kwenye bidhaa, amesema alikuwa hajui kama sheria inamtaka kufanya hivyo. Hata hivyo, Waziri Saada amekataa sababu hiyo, akisema huo umekuwa mchezo wa siku nyingi na wengi hujificha katika kichaka hicho.
Katika baadhi ya maduka yaliyofanyiwa ukaguzi, baada ya kukagua mashine za kielektroniki, ilibainika kuwa mara ya mwisho risiti ilitolewa Machi mosi kwa bidhaa ya Sh52,000.