
MSHAMBULIAJI wa Dodoma Jiji, Wazir Jr Shentembo amejiunga na Al Mina’a FC inayoshiriki Ligi Kuu ya Iraq akimfuata Simon Msuva anayekipiga katika timu ya Al Talaba.
Wazir Jr ambaye aliwahi kukipiga Yanga 2020/21, amesaini mkataba wa miezi sita kujiunga na timu hiyo iliyopo nafasi ya 16 kwenye msimamo wa ligi hiyo yenye timu 20.
Akizungumza na Mwanaspoti, Katibu Mkuu wa Dodoma Jiji, Fortunatus Johnson alisema nyota huyo amejiunga na chama hilo kwa mkopo na mwisho wa msimu watakaa na kuangalia namna ya kuboresha maslahi yake kwa kuwa atarejea katika kikosi hicho.
“Ameshaondoka tangu Februari 7, yupo kwa mkopo baada ya miezi sita tutaangalia namna gani ya kuboresha maslahi ya nyota huyo,” alisema Fourtunatus na kuongeza:
“Timu hiyo ilimuona alipokwenda kufanya trial (majaribio) nchini Brunei ambako kulikuwa na mawakala mbalimbali, baada ya timu ya nchi hiyo kuchelewa (kumsajili) Mina’a ikamsajili.”
TAKWIMU ZA WAZIR BARA
Msimu wa 2015/16 na 2016/17 akiwa na Toto Africans alifunga mabao 14 ilhali uliofuata akatua Azam FC na kufunga bao moja, msimu 2018/19 (Biashara United) mabao matatu.
Akiwa Mbao FC, Waziri Jr alifunga mabao 14 kwenye mechi 12 msimu 2019/20 ndipo Yanga ikamsajili uliofuatia akafunga mabao mawili, 2021/22 mabao manne Dodoma Jiji akacheza misimu miwili KMC na kufunga mabao 13.
Kwa msimu huu katika Ligi Kuu akiwa na Dodoma Jiji, nyota huyo amefunga bao moja katika pambano lililopigwa Oktoba 2, 2024 ambapo Dodoma iliizima Tabora United kwa mabao 2-0, Wazir akifunga la pili katika dakika za majeruhi, huku la kwanza likiwekwa kimiani na Paul Peter dakika ya 46.